ONSPOT MAGAZINE

ONSPOT MAGAZINE

‘WANANCHI SAME MASHARIKI WAMEKATA TAMAA’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MWANAHARAKATI na mdau wa maendeleo ya wananchi wa Same Mashariki, Allan Mmanyi ‘Mkombozi’ amesema hali ya maisha ya wakazi wa vijiji vingi vya Same Mashariki inasikitisha kwa kuwa wengi wao wamekata tamaa.
Mkombozi anayefuatilia kwa karibu maisha ya wananchi wa eneo hilo mkoani Kilimanjaro, ameliambia gazeti hili kuwa kila siku watu wa Same Mashariki hushukuru Mungu kwa kusema afadhali ya jana kwani, kilimo kama nguzo kuu ya kiuchumi kwao, kimekuwa hakiwaletei tija yoyote.
“Ni hatari ukifika vijiji vya Vuje, Maore, Ndungu, Bombo, Mvaha na milimani ukawauliza wakulima wanachohitaji utawasikia wakilalamika shida yao ni ukosefu wa soko la uhakika la mazao na uhaba wa pembejeo.
“Hawajui nani atawajibika kuwalipa japo fidia kidogo ya hasara waliyopata. Kwa kweli ni ukatili uliopitiliza ambao watu wa Gonja milimani wanafanyiwa… upande wa elimu, ni shida shule chache, walimu hawatoshi, maabara hakuna huku umbali ukiwa kikwazo kwa wanafunzi wa baadhi ya maeneo," alisema.
Alisema anajipanga kufanya mapinzudi ya kilimo na kwamba ameandaa mpango wa kuwawezesha wana Same Mashariki kuepukana na adha hiyo kwa kubuni njia mbadala za kilimo chenye tija.
Chanzo;Tanzania Daima

TAKUKURU YAOKOA BILIONI 38.9/

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema imeokoa zaidi ya Sh bilioni 38.9 zilizotarajiwa kuingia katika mikono ya wajanja wachache kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema fedha hizo zimerejeshwa Hazina kutekeleza shughuli nyingine za maendeleo.
Dk Hoseah alisema kiasi hicho ni ongezeko la Sh bilioni 33.59, ikilinganishwa na fedha zilizookolewa mwaka mmoja uliopita.
Alisema hayo kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa taasisi kutoka mikoa yote nchini, unaofanyika mjini hapa.
Alisema fedha hizo zimeokolewa, kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, inayotekelezwa katika mikoa tofauti nchini.
Alisema baadhi ya watendaji walikusudia ziingie katika mifuko yao.
"Tutaendelea kuokoa fedha zinazofujwa na wajanja wachache, vilevile katika kipindi hicho tumefungua kesi 327 zikiwamo tatu kubwa zinazohusu viongozi mbalimbali serikalini, waliojihusisha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa taratibu," alisema.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama alitaka taasisi hiyo kujitathmini kwa kazi wanayofanya kama inakidhi mahitaji ya wananchi katika suala zima la kukabili vitendo vya vilivyokithiri sekta ya afya, elimu na miundombinu.
"Natambua kazi kubwa mnayofanya lakini naomba muongeze kasi kupambana na wala rushwa wakubwa ambao wameona kwamba rushwa ni sehemu ya haki yao...hii haiwazuii kuendelea kuwadhibiti wala rushwa wadogo, serikali inathamini mchango wenu," alisema Gama.
Chanzo;Habari Leo 

MEYA WA CHADEMA ASUSIA MBIO ZA MWENGE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

MEYA wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Japhary Michael kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesusia kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru katika manispaa anayoiongoza.

Kutokana na kitendo hicho, kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Bi.Rachel Kasanda, alidai kusikitishwa na hali hiyo akisema Michael hakuwatendea haki wananchi anaowaongoza.

"Mwenge huu si wa chama chochote cha siasa bali hii ni nembo ya Taifa, upo kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya wananchi," alisema.

Alisema pamoja Michael kushindwa kutoa ushirikiano, mbio za Mwenge huo zimezindua barabara ambayo ipo Mtaa wa Shahili anaoishi Meya huyo ambako ana nyumba na duka labiashara.

"Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi yake kutoshiriki katika mbio za Mwenge nchini tangu ulipowashwa Mei 2 mwaka huu na Makamu wa Rais, Dkt. Mohamed Gharib Bilal Mjini Bukoba, mkoani Kagera," alisema.

Bi. Kasanda alisema, Meya huyo hakupaswa kususia Mwenge wa Uhuru ambao unaleta maendeleo kwa Watanzania na barabara iliyozinduliwa katika mtaa huo inatumika na watu wote bila kujali itikadi ya vyama vya siasa, rangi au dini.

Hata hivyo, Michael ambaye baada ya uzinduzi wa barabara hiyo alikuwepo dukani kwake, alisema amewakilishwa na madiwani watatu wa chama chake.

Alisema msafara wa Mwenge ulikuwa na madiwani wengine wa CHADEMA akiwamo Diwani wa Kata ya Kiusa, Stephen Ngasa hivyo hapakuwa na ulazima wa yeye kuwepo.

 Chanzo;Majira

WANANCHI MABUNGO WATAKIWA KULIMA MTAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

WANANCHI wa Kijiji cha Mabungo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro,wametakiwa kulima mazao yanayostahimili hali ya ukame ikiwemo mtama,hatua ambayo itawawezesha kuondokana na tatizo la njaa ambalo limekuwa likiwakumba kila mwaka kutokana na upungufu wa mvua.

Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Eliahidi Mvanga, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kijiji ulioenda sambamba na maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi ambapo alisema moja ya mikakati waliyonayo katika kijiji hicho, ni uhamasishaji wa Kilimo cha mtama.

Mvamba alisema kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo sasa, wananchji wa kijiji hicho wamekuwa wakitegemea chakula cha msaada kutokana na mazao yao kukauka kwa kukosa mvua za kutosha, hivyo ni wakati wa wananchi kuondokana na kilimo cha mazoea na kuhakikisha wanalima mtama ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo.

"Hali ya ukame imetuathiri kwa kiasi kikubwa wananchi wa Mabungo, na kutokana na hali hii wilaya imetoa agizo wananchi wa maeneo ya ukanda wa chini walime mtama angalau robo heka kila mmoja, na sasa niwatake wananchi, mtekeleze agizo hili na ikiwezekana mlime hata heka moja, ili kuweza kuondokana na tatizo hili la njaa ambalo limekuwa likitusumbua kila mwaka"alisema Mvamba.

Alisema mtama nizao la chakula na biashara, hivyo wananchi wakilima zao hilo wanaweza pia kuondokana na tatizo la umaskini na kufanikiwa kuwapeleka watoto wao shule bila shida wala usumbufu.

"Wananchi wa eneo hili wengi wetu tunategemea kilimo kuyaendesha maisha yetu ya kila siku, sasa mnapaswa kutambua kuwa mtama ni zao la chakula na biashara, na endapo mtaitikia wito huu na kulima zao hili kwa wingi na kwa utaalamu, tutafanikiwa kuwasomesha watoto wetu hadi vyuo vikuu bila usumbufu"alisema.

Mwenyekiti huyo alisema, pamoja na jitihada mbalimbali ambazo wamekuwa wakizifanya katika kuhakikisha wanainua sekta ya kilimo katika kijiji hicho,bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa pembejeo, hali ambayo imekuwa ikiwafanya wakulima wengi kuendeleza kilimo kisicho na tija.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa pembejeo katika kijiji hicho lakini ni chache ikilinganishwa na mahitaji halisi ya wananchi, hivyo kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwaongezea pembejeo, ili kuweza kulima kilimo cha kisasa na ambacho kitawakwamua wananchi kiuchumi.

Wakizungumza baadhi ya wananchi wa kijiji hicho,walisema suala la pembejeo limekuwa ni tatizo kubwa, kutokana na kwamba ambazo zimekuwa zikitolewa na Serikali ni chache sana ambazo hazitoshelezi.

Raihana Shaban aliiomba Serikali kuwaongezea pembejeo za ruzuku,ili kuwawezesha wananchi wote kupata na kuondokana na kilimo cha mazoea.

Chanzo;Majira

NDEGE YAKWAMISHA KESI YA MBOWE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Jimbo la Hai,Freeman Mbowe
 
Kesi ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe, iliyotarajiwa kusikilizwa jana katika mahakama ya Wilaya ya Hai, imehairishwa  baada ya  mstakiwa huyo kushindwa kufika mahakamani.
Ilidaiwa kuwa Mbowe alishindwa kufika hapo kutokana na kuachwa na ndege.

 Akizungunza mbele ya hakimu Agnes Muhina  mdhamini wa Mbowe, Awazi Urono, alisema mwenyekiti huyo  alishindwa  kufika baada ya ndege aliyotarajia kusafiria kumuacha.

“Mheshimiwa hakimu,  Mbowe  ameshindwa kufika mahakamani kwa sababu gari lake limepata hitilafu wakati akielekea uwanja wa ndege (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere-JNIA)…Aliachwa na ndege iliyokuwa inakuja KIA kwa hiyo naomba ichukuliwe kama udhuru na taarifa rasmi ya mahakama,” alisema Urono.

NIPASHE ilishuhudia mahakamani hapo wananchi  wakifurika kwa lengo likiwa  kusikiliza kesi ya Mbowe anadaiw akumshambulia Nassir Yamin ambaye alikuwa ni mwangalizi wa ndani katika uchaguzi huo.  Baada ya taarifa hiyo,   Hakimu Muhina alisema mahakama imepokea rasmi ujumbe huo kama taarifa ya mahakama na kwamba  kesi hiyo imeahirishwa mpaka Novemba 8, mwaka huu.

“Kwa kuwa mdhamini wa Mbowe yupo, dhamana ya mshitakiwa inaendelea kama kawaida,  lakini pia naamini upande wa utetezi umejipanga vizuri kuhusu mashahidi na vielelezo.,” alisema Hakimu Muhina

Katika kesi hiyo ya jinai namba 73 ya mwaka 2011,  Mbowe akiwa mmoja kati ya wagombea ubunge wa jimbo la Hai, anadaiwa kumshambulia Nassir Yamin katika Kijiji cha Nshara, Kata ya Machame Kaskazini, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro

Katika uchaguzi huo, Mbowe aliibuka mshindi kwa kupata kura 28,585 akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM) kura 23,349,  Hawa Kihogo (UDP) kura 258 na Petro Kisimbo (TLP) 135.
CHANZO: NIPASHE

DKT. MALASUSA AVUNJA UKIMYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WAKATI Taifa likiwa katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt.

Alex Malasusa, amesema Kanisa hilo halipo tayari kuvumilia mifumo inayominya haki za wananchi na uhuru wa kuishi kwa amani.

Dkt. Malasusa aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha neno kuu katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo unaoendelea katika Chuo Kikuu cha Stephano Moshi (SMMUCO), kilichoko mkoani Kilimanjaro.

Alisema jamii inayoongozwa na mifumo ya uonevu, hupoteza uzalendo ambapo nchi yenye mifumo ya namna hiyo, kauli ambazo hutumika ni zile za ‘mwenye nguvu mpishe apite’.

“Wenye nguvu huishi bila huruma wala chembe ya ubinadamu kwa wenzao wanyonge...Kanisa haliwezi kuwa kimya kwa mifumo ya aina hii, hata sasa kuna taarifa mbalimbali zinazodai mwenye fedha au uwezo wa aina yoyote, akikamatwa hakai ndani huachiwa mapema kutokana na uwezo wake kifedha ukilinganisha na wanyonge,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika mifumo ya namna hiyo kwenye maisha, mwenye nguvu au uwezo akikosea badala ya kuchukuliwa hatua zinazostahili, yeye ndiye anayeamua hatima ya kosa alilolifanya ambapo mifumo ya namna hiyo, husababisha nchi kukosa mwelekeo na watawala kukosa misimamo thabiti.

Alitoa wito kwa waumini wa Kanisa hilo na Watanzania wote, kutokata tamaa kutokana na hali ngumu ya maisha akiwataka wazidi kuliombea Taifa liweze kuendelea na hali ya utulivu uliopo.

“Kama ilivyokuwa enzi za Yohana wa Patimo, jamii yetu kwa sasa inapitia Patimo nyingi yenye maisha magumu, maadili yameporomoka, utamaduni wetu umeanza kuporomoka na heshima imetoweka, kilichobaki ni kumwomba Mungu na kumtegemea ili turudie hali ya uwepo wa maadili mema”, alisema.

Akizungumzia maombezi na huduma zingine za Kanisa, Askofu Dkt. Malasusa alisema kuna baadhi ya watu wamegeuza suala la maombi kuwa duka la kujipatia mapato.

“Wakati wa mateso na shida mbalimbali zinazomkabili mwanadamu,hutokea watu wanaojidai Manabii na Mitume, uzalendo hutoweka na jamii kuongozwa kwa vitisho,” alisema.

Kuhusu utandawazi, alisema pamoja na nia njema ya kukua kwa teknolojia, baadhi ya watu wameamua kuitumia vibaya fursa hiyo kutokana na kutoandaliwa vizuri katika kupokea teknolojia husika.

“Kuna watu ambao huingia Kanisani na simu na kuanza kuitumia katika kufuatilia Ibada kwa sababu ya kuhifadhi maandiko ya Biblia

Takatifu kwenye simu zao... pamoja na mawazo yao mazuri huwa inaondoa maana halisi ya ushiriki katika Ibada, si dhambi kufanya hivyo ila si mwenendo mzuri,” alisema.

Mkutano huo unaotarajiwa kumalizika kesho umekuwa ukiongozwa na neno kuu linalosema; “Tazama nayafanya yote kuwa mapya”.

 Chanzo;Majira

JWTZ YAZINDUA ZOEZI KUBWA LA KIVITA MONDULI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kikosi cha Ardhini cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikiwa kwenye mazoezi maalumu katika kambi ya Msangani, iliyoko Kibaha, mkoani Pwani jana. Kikosi hicho na vikosi vingine vya jeshi hilo vinafanya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya JWTZ yatakayofanyika Monduli, Arusha Sepemba 5, mwaka huu. PICHA: NDENINSIA LISLEY
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limezindua zoezi kubwa la kivita linayoishirikisha Divisheni moja ya kijeshi.
Zoezi hilo linalofanyika katika eneo la Monduli, mkoani Arusha, ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa JWTZ Septemba mosi, 1964.

Divisheni hiyo inaundwa na makamanda na wapiganaji kutoka Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Akiba.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi, aliwataka washiriki kutumia weledi wao kwa umakini ili malengo ya zoezi hilo ya medani yafikiwe.

“Hili ni la muhimu katika kulifanya jeshi letu liwe katika hali ya utimamu na uwezo mzuri wa kimapigano,” alisema.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema madhumuni ya mazoezi hayo, pamoja na mambo mengine, ni kupima na kujenga uwezo wa utendaji wa pamoja wa JWTZ katika kukabiliana na adui kivita, kwenye nchi kavu na anga.

“Zoezi hili linalenga kuinua uwezo wa kupanga na kutekeleza jukumu la kivita kwa makamanda na askari wetu katika zoezi la pamoja, kujiweka tayari kukabiliana na adui halisi, na kupima uwezo wa uhamasishaji na usambaratishaji na mengineo,” alisema

Naye Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu na aliye Kamandi Mkuu wa zoezi hilo, Meja Jenerali Salum Kijuu, alisema zoezi hilo linahusisha silaha mpya na zana mbalimbali za kimapigano kama ndege vita, vifaru na magari ya delaya.

“Lakini pia wahandisi na vikundi vya lojistiki na litakamilika kwa kufanya shambulio la kukusudia,” alisema. Kwa mujibu wa Meja Jenarali Kijuu, zoezi hilo lililoanza jana linatarajiwa kumalizika Septemba 5, mwaka huu.
SOURCE: NIPASHE

MSUYA;MCBL IWE BENKI YA BIASHARA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Benki ya Wananchi Mwanga (MCBL)WAZIRI Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya ameushauri uongozi wa Benki ya Wananchi Mwanga (MCBL) kuibadili kutoka benki ya wananchi na kuwa ya biashara ili ya kupanua wigo na kufungua matawi kwenye mikoa mingine.
Msuya alitoa ushauri huo hivi karibuni alipokuwa akichangia namna ya kuifanya MCBL kukua katika mkutano mkuu wa 14 wa mwaka uliofanyika wilayani Mwanga, Kilimanjaro.
“Ningependa kushauri MCBL ibadilishe utoaji huduma zake kutoka benki ya wananchi na kuwa benki ya biashara… itasaidia kupanua wigo wake na kufungua matawi mikoani,” alisema.
MCBL ilitangaza mafaniko yake kibiashara kwa kupata faida ya sh milioni 68 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 licha ya changamoto nyingi zinazoikabili.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima jana  Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Abby Ghuhia, alisema faida ya mwaka 2013 imeshuka ikilinganishwa na mwaka 2012 kutokana na gharama za uendeshaji kuongezeka baada ya kufungua vituo vya huduma Moshi Mjini na Same.
Aliongeza kuwa mtaji wa hisa umeongezeka kutoka  sh milioni 555 hadi sh milioni 567 sawa na ongezeko la sh milioni 12.
 Chanzo:Tanzania Daima

KIRUA VUNJO NORTHAMCOSKUPATA MILIONI 4.8/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

CHAMA cha ushirika wa masoko na mazao ya kilimo cha Kirua Vunjo Kaskazini, (Kirua Vunjo North Amcos), cha Moshi Vjijini, mkoani Kilimanjaro, kinatarajia kupata mapato ya ziada ya sh. milioni 4.8, katika msimu wa 2014/2015.

Hayo yameelezwa na mwenyekiti wa chama hicho Bw. John Chaki, wakati akizungumza na wanahabari, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, hivi karibuni.

"Ziada hii itatokana na mapato ya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 15 tunayotarajia kuyapata katika kipindi hiki," alisema na kuongeza kuwa wanachama wa chama hicho tayari wameridhia kujiunga na mfumo mpya wa kukusanya kahawa kwa kujitegemea.

Aliongeza, "Ili kufanikisha zoezi la kujitegemea katika mfumo huu mpya, wanachama wamepitisha ukomo wa madeni wa shilingi milioni 120 kutoka benki ya ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL), kwa ajili ya kukusanyia kahawa katika msimu huu mpya."

Awali meneja masoko wa KCBL Bw. Asanterabi Msigomba, alisema benki hiyo tayari imeshaandaa mikakati inayolenga kuviwezesha vyama vya ushirika wa masoko na mazao ya kilimo vilivyojiunga na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.

Aidha alitoa wito kwa vyama vya ushirika masoko na mazao ya kilimo kujenga tabia ya kuwalipa wakulima fedha zao punde wanapowasilisha mazao yao ili waweze kujiendeleza ikiwamo kulipa fedha walizokopa kwa ajili ya kuimarisha kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.

"Kosa kubwa ambalo linaweza kudhoofisha juhudi za kilimo ni kutokumlipa mkulima kwa wakati na wakulima kuuza mazao nje ya mfumo wa chama, mambo haya hudhoofisha mfumo mzima unaolenga kuongeza tija katika kilimo," alionya.

Bw. Msigomba pia alielezea umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ulioasisiwa na benki hiyo ya kwanza ya ushirika hapa nchini ambapo alisema tayari taasisi hiyo ishatoa mafunzo kwa vyama vya ushirika wa masoko na mazao ya kilimo (Amcos), kuhusu mfumo huo.

Chanzo:Majira

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa