Home » » DC Hai ageuka mbogo kwa wanaokata miti

DC Hai ageuka mbogo kwa wanaokata miti



 
Na Eliya Mbonea, Hai
MKUU wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Novatus Makunga, ametangaza vita dhidi ya viongozi wa ngazi za vijiji, vitongoji na wananchi wanaoshiriki vitendo vya kukata miti.

Akizungumza wilayani humo hivi karibuni, Makunga alisema pamoja na kuzuiwa kwa vibali vya ukataji miti, bado wameendelea kukumbana na vikwazo kutoka kwa baadhi ya viongozi. 

“Uamuzi huu ni mgumu, unalenga kuokoa maisha ya watu, lakini wapo baadhi ya viongozi vijijini na vitongoji wanaendelea kushiriki ukataji wa miti.

“Wananchi kwa kushirikiana na askari wetu wa mgambo tunawaomba tushirikiane kuwafichua watu hawa na tukifanikiwa kuwakamata na kujiridhisha sheria itachukua mkondo wake,” alisema Makunga.

Alisema hivi sasa wilayani hapo ipo operesheni kabambe ya kurejesha mazingira yake kuwa katika hali ya asili kwa kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi.

Alisema wananchi na viongozi wilayani Hai wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha mazingira ambayo miaka ya karibuni yameharibiwa kwa ukataji ovyo wa miti.

“Tunalo jukumu la kuhakikisha mazingira yanarejea kwenye uoto wake wa asili, huu ni wajibu wetu, ikichukuliwa kuwa tupo jirani kabisa na Mlima Kilimanjaro,” alisema Makunga.

Alisema katika kutimiza majukumu hayo, wanazo kazi za kufanya, ikiwa ni kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya ukataji wa miti kwa ajili ya magogo na mbao.

“Sasa kwa kuwa tumesitisha ukataji wa miti, inabidi tuhakikishe jukumu la pili la kupanda miti kwa kasi kubwa linafanyika kwa haraka na kiwango cha juu,” alisema Makunga.

Alisema kutokana na majukumu hayo hivi sasa wana kila sababu ya kuhakikisha askari mgambo wilayani humo wanawaondoa wavamizi wa vyanzo vya maji, kingo za mito na maeneo ya ardhi oevu.

Alisema tayari mchakato huo umeanza kwa kuainisha maeneo yote, huku baadhi ya maeneo wakiwa wamekwisha kutoa notisi ya kuwataka watu wanaoendesha kilimo baada ya mavuno kuacha kuendelea na kilimo katika msimu ujao.

“Ninyi mnafahamu wananchi wenzetu hapa wanaendesha kilimo, hasa cha miwa mpaka ndani ya mita sitini kutoka katika kingo za mito na katika vyanzo vya maji.

“Pamoja na kuwaondoa tuna mkakati wa kuweka mawe ya alama kwa ajili ya kuonyesha mwisho wa shughuli za kibinadamu katika mito na vyanzo vya maji,” alisema Makunga.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa