WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, juzi aliongoza mhadhara unaohusu
maendeleo ya Bara la Afrika katika Chuo Kikuu cha Columbus, jijini New York,
nchini Marekani.
Katika mhadhara huo, Bw. Sumaye alichambua kwa kina masuala mbalimbali
yanayopaswa kupewa kipaumbele ili kuharakisha maendeleo barani Afrika.
Hatua ya Bw. Sumaye kuongoza mjadala katika mhadhara huo wa Kimataifa,
inatafsiriwa ni moja ya kazi zinazochukuliwa na makada wanaotajwa kutaka
kugombea urais kama njia moja wapo ya kujiongezea sifa kitaifa na kimataifa.
Wakati Bw. Sumaye akiibukia nchini humo, wanasiasa wengine wanaotajwa katika
kinyang'anyiro hicho wamekuwa wakishiriki shughuli mbalimbali za kijamii nchini
na kutoa misaada.
Hiyo ni safari ya pili kwa Bw. Sumaye kualikwa kutoa mihadhara kwenye vyuo
vikuu mbalimbali nchini Marekani ambapo awali alifanya ziara kama hiyo na kutoa
mhadhara katika vyuo vikuu kikiwemo Chuo Kikuu cha Harvard, alikosomea.
Hatua ya kualikwa mara kwa mara katika vyuo vilivyopo katika nchi za Magharibi,
inaonesha huenda kuna uungwaji mkono kwa namna moja ama nyingine kutoka nchi
hizo.
Bw. Sumaye alisema, nchi za Afrika zinatakiwa kujipanga upya na kuongeza
ushirikiano ili kutumia zaidi masoko ya ndani badala kutegemea masoko ya nje
yenye ushindani mkubwa na ukatili.
Alisema nchi nyingi za Afrika zimekuwa zikifanya biashara zaidi na nchi za
Magharibi au Mashariki lakini zimekuwa zikikosa ushindani kutokana na kuwekewa
vikwazo mbalimbali hususan viwango vya ubora na ujanja mwingine.
"Kama nilivyosema awali, ugawaji uliofanywa na wakoloni, kuzigawa nchi za
Afrika katika mataifa madogo kulisababisha madhara makubwa mawili katika uchumi
wa bara hili.
"Moja ni kuendelea na utegemezi kwa wakoloni wa zamani, pili ni udhaifu
kutokana na udogo wa nchi," alisema Bw. Sumaye na kuongeza kuwa, ili
kuondokana na matatizo hayo nchi za Afrika lazima zijenge msingi wake
imara na kufanya kazi kwa pamoja kuanzia eneo hilo.
Aliongeza kuwa, nchi za Afrika lazima zijitambue kuwa ni dhaifu sana katika
masuala ya kiuchumi akisema umefika wakati wa kuunda umoja wao ambao utakuwa na
nguvu ya kuinua uchumi wa nchi hizo.
Bw. Sumaye alisema, kama nchi hizo zitafanikiwa kujiunda katika makundi ya
kikanda, itazisaidia kuwa na sauti ya pamoja katika kuimarisha uchumi wake.
"Nchi nyingi za Afrika zinashindwa kufanya biashara zaidi na nchi za
Magharibi au Mashariki kutokana na vikwazo vya ubora wa bidhaa
wanavyowekewa," alisema.
Aliongeza kuwa, nchi hizo zina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa nyingi
zinazoweza kuleta ushindani katika masoko ya kisasa duniani ambapo upangaji
upya katika makundi ya kiuchumi kama ECOWAS, Jumuiya ya Afrika Mashariki-EAC,
SADC, COMESA, unaweza kuwa jambo muhimu katika kuimarisha uchumi wa Afrika.
Alishauri sekta binafsi ilindwe na ipewe umuhimu unaostahili na kulinda viwanda
vichanga ambapo akizungumzia sera za uwekezaji, alishauri ziangaliwe upya ili
ziwalinde wawekezaji, kulinda masilahi ya nchi na wananchi kwani baadhi ya sera
hizo zimewekwa kutokana na ushawishi wa wakubwa kwa masilahi yao.
Upande wa elimu, alisema usomi ni pamoja na kujitoa mhanga kwa ajili ya
wengine, kuwa na uzalendo wa kweli ambapo wasomi
wasitumike kuondoa uchumi mbovu na umaskini hivyo lazima Afrika ikubali
mabadiliko ya fikra.
Chanzo Gazeti la Mwananchi.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment