SERIKALI imesalimu amri baada ya tishio la
wazalishaji wa sukari nchini kufunga viwanda vyao iwapo hatua madhubuti za
kukabiliana na uingizwaji holela wa sukari kutoka nje ya nchi bila kulipiwa
ushuru, hazitachukuliwa.
Baada ya tishio hilo serikali sasa imekusudia
kuitisha mkutano wa wazalishaji, wawekezaji, wafanyabiashara wanaoingiza sukari
hiyo na walaji ili kujadili changamoto ya kufurika kwa sukari ya nje katika
soko la ndani.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher
Chiza, alisema kutokana na changamoto hiyo wizara yake inakusudia kuandaa
mkutano wa kitaifa ili kutafuta namna sahihi ya kulikabili jambo hilo.
Chiza alisema lengo la mkutano huo ni kujenga
mazingira rafiki na kuridhisha kila upande kwani lengo ni kuhakikisha viwanda
vya ndani vikiendeleza uzalishaji wake huku vikitoa ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji na Utawala wa
Kiwanda cha Sukari Moshi (TPC) Jafary Ali alisema kiwanda chake kimelazimika
kuomba maghala binafsi kwenye mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ili kuhifadhi
sukari yao.
Alisema uwezo wa kiwanda ni kuhifadhi tani 13,000
kwa wakati mmoja lakini hadi sasa wamezalisha tani 20,000 na kulazimika kuomba
kuhifadhiwa tani 7,000 baada ya kukosa soko la ndani.
Ofisa huyo alisema sukari inayozalishwa nchini
inauzwa kwa wastani wa sh 69,000 hadi sh 75,000 kwa mfuko wa kilogramu 50
wakati sukari inayotoka nje inauzwa kwa sh 50,000 kwa mfuko wenye ukubwa hiyo
jambo linalosababisha sukari ya ndani kukosa soko.
Kwa mujibu wa Ally hivi sasa ipo sukari inayoingia
kwa wingi katika soko ijulikanayo kama ‘sukari isiyolipiwa kodiambayo haina
vibali vya bodi ya sukari na kutaka serikali inapaswa kujua inaingiaje.
“Kuna sukari nyingine inakuja kwa ajili ya matumizi
ya viwanda ambavyo havitumii ‘brown sugarsasa hii ‘industrial sugarinakuja kwa
ujanja; ujanja unatumika badala ya kuleta sukari nyeupe kwa ajili ya matumizi
ya viwanda wanaleta sukari kama ile tunayozalisha nchini,” alisema.
Alitaja aina ya sukari inayoingizwa nchini kuwa ni
‘Transit Sugarinayopitishwa nchini kwenda nchi za Burundi, Rwanda na Congo na
kwamba baadhi ya wanatumia ujanja kuisambaza katika soko la Tanzania.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa kipindi cha
mwezi mmoja sasa, umebaini kuwepo kwa ongezeko la sukari inayoingizwa nchini ambayo
ni zaidi ya tani 200,000 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment