MAMLAKA ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) imeombwa
kutanua wigo wa kufanya shughuli zake za ukaguzi hadi kwa watengenezaji wa
pombe za kienyeji katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ili kupunguza madhara
mbalimbali yanayowapata watumiaji.
Mbali na ombi hilo pia serikali imeombwa
kurasimisha vibali kwa watengezaji wa pombe za kienyeji katika mikoa hiyo ili
kujiongezea kipato sanjari na kupunguza malalamiko toka kwa wazalishaji wengine
wa vileo wanaofuata sheria kuchafuliwa katika soko.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mawakala wa
kampuni ya Banana Investment ya jijini Arusha, mkurugenzi wa kampuni hiyo,
Adolf Olomi, alisema asilimia 90 ya watengezaji pombe za kienyeji
hawajathibitisha bidhaa zao TFDA hali inayochangia pia kuuza bidhaa zao kwa bei
ya chini.
“Bidhaa yoyote kwa ajili ya kula ama kunywa ambayo
imetengenezwa ndani au nje ya nchi lazima ithibitishwe na TFDA kabla ya
kuruhusiwa kuuzwa katika soko la Tanzania, kwa watengenezaji wa pombe za
kienyeji asilimia 90 hawajaenda kuthibitisha bidhaa zao,” alisema Olomi.
Alisema iwapo vyombo vya serikali vinahitaji
kutunza afya ya wananchi ni wajibu wa vyombo husika kuwatafuta watengenezaji wa
pombe za kienyeji wathibitishe kama zinastahili au la.
“Tunafahamu wengi wao si rasmi kwa sababu
hawajajisajili katika vyombo husika kama vile vya kulipa kodi na leseni hivyo
gharama zao za uendeshaji zinakuwa kidogo kutokana na kwamba hawalipi gharama
zile stahiki kwa vyombo husika,” alisema Olomi.
Alisema kutokana na kutokuwa na gharama katika
uzalishaji wao hupelekea kuuza bidhaa zao kwa bei ya chini hatua inayochangia
kutokuwepo kwa ushindani sawa katika soko la bidhaa hizo kwa watengenezaji
wengine wanaofuata sheria.
Olomi alisema kampuni yake iko kwenye mkakati wa
kufanya operesheni ya kuwakamata watengenezaji wa pombe za kienyeji ambao
wamekuwa wakitumia vifungashio vya kampuni hiyo zikiwemo nembo pamoja na
makasha kuweka bidhaa hafifu.
“Tuna mpango wa kuwatumia Majembe Auction Mart kwa
ajili ya kuwakamata wote wanaotengeneza pombe za kienyeji na kisha kuziweka
katika chupa na makasha yetu kwa lengo la kuwaaminisha watumiaji wa kinywaji
hicho kuwa ndicho halisi kutoka katika kiwanda cha Banana,” alisema Olomi.
Naye meneja masoko wa kampuni hiyo David Damian
alisema Banana Investment imetoa zawadi kwa mawakala waliofanya vizuri katika
mauzo mkoa wa Kilimanjaro.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment