✔️VIJIJI 506 VIMEUNGANISHWA NA UMEME KATI YA VIJIJI 519 SAWA NA 97.49%
Serikali
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa kiasi cha Shilingi
Bilioni 23.7 ili kuhakikisha miradi yote ya kusambaza umeme vijijini
Mkoani Kilimanjaro inakamilika na kuwapatia wananchi maendeleo ya
kiuchumi na kijamii
Mkurugenzi
wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amebainisha hayo mbele ya
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa Julai 29 Mkoani
Kilimanjaro wakati wa utambulisho wa Wakandarasi walioshinda tenda ya
kusambaza umeme katika vijiji 13 vilivyokuwa vimesalia.
"Hadi
sasa tumeunganisha umeme katika vijiji 506 kati ya vijiji 519 ambayo ni
sawa na asilimia 97.49 Mkoani hapa; na leo hii tupo hapa kutambulisha
Wakandarasi watakaotekeleza miradi katika vijiji hivi vilivyosalia,"
amebainisha Mhandisi Olotu.
Mhandisi
Olutu amebainisha kuwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro REA inatekeleza jumla ya
miradi mikubwa mitatu ambayo ni mradi wa shilingi bilioni 13.1 wa
kusambaza umeme vijijini, mradi wa bilioni 8.8 wa kusambaza umeme kwenye
migodi midogo na maeneo ya kilimo na mradi wa bilioni 1. 7 wa kusambaza
umeme katika vituo vya afya na visima vya maji.
"Tumefika
hapa kwa lengo la kutambulisha Wakandarasi watakokamilisha kazi
iliyobaki Mkoani hapa sambamba na kutambulisha wasimamizi wake kwa
upande wa REA ambao miongoni mwa majukumu walionayo ni kuwasilisha kwako
taarifa za mara kwa mara za maendedeleo na hatua za utekelezaji,"
amefafanua Mhandisi Olotu.
Akizungumza
wakati wa utambulisho wa wakandarasi hao; Katibu Tawala wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Kiseo Nzowa ameipongeza REA kwa kuendelea kufanikisha
dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia umeme.
"Umeme
ni injini ya uchumi wa taifa lolote duniani na kwakutambua hilo,
Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi katika
Sekta ya Nishati na kwa bahati nzuri REA mmetambua vyema dhamira ya Mhe.
Rais na mnatekeleza kwa vitendo," amepongeza Nzowa.
Aidha,
amewataka Wakandarasi waliopewa jukumu hilo la kufikisha umeme katika
vijiji vilivyosalia kufanya kazi kwa weledi na kwa kasi ili kukamilisha
na kukabidhi mradi ndani ya muda uliopangwa.
"Wote
mliopewa jukumu ni wazawa; hatutarajii kuona kazi ikikwama; kukitokea
changamoto yoyote Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ipo wazi kuwasikiliza na kusonga
mbele," amesisitiza Nzowa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Wakandarasi hao waliahidi kufanya kazi kwa weledi,
ubunifu na kasi ili kutimiza dhamira ya Serikali.
"Serikali
imetuamini kwa kutupa kazi, nasi tunaahidi kuhakikisha hatufanyi
makosa; tutatekeleza kazi hii kwa uzalendo ili sote kwa pamoja tutimize
dhamira ya Rais wetu," amesema Mhandisi Cuthbert Shirima, Mkandarasi
kutoka Kampuni ya Transpower Limited.
Kampuni
zilizopewa jukumu la kukamilisha vijiji 13 vilivyosalia Mkoani humo ni
Northern Engineering works Ltd (Wilaya ya Hai), Radi Services Ltd
(Wilaya ya Hai na Moshi), Transpower Ltd (Wilaya ya Same) na Octupus
Engineering Ltd (Wilaya ya Mwanga).