Home » » Bwawa la Nyumba ya Mungu hatarini kukauka

Bwawa la Nyumba ya Mungu hatarini kukauka


Na Upendo Mosha, Mwanga
BWAWA la Nyumba ya Mungu lililopo wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, ambalo linategemewa kwa shughuli za uzalisahaji umeme na umwagiliaji ni mbaya, kutokana na maji kupungua kutoka mita za ujazo bilioni 1.1 hadi kufikia mita milioni 300 kutokana na ukosefu wa mvua.

Hayo yalibainishwa na Kaimu Afisa Maji Bonde la Pangani, Jerobuam Riwa, wakati wa kutembelea bwawa hilo na kusema upungufu huo, umetokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na wanadamu katika vyanzo vya maji na misitu.

Alisema bwawa hilo, limekuwa likitegemewa katika shughuli mbalimbali za uzalisha, ikiwemo ufuaji umeme pamoja na umwagiliaji.

Alisema kutokana na hali hiyo, Serikali kama haitachukua hatua za haraka kulinusuru bwawa hilo, hali itazidi kuwa mbaya kuliko ilivyo sasa.

Alisema kutokana na tatizo hilo, tayari ofisi ya bonde hilo imeanza utaratibu wa kuzungumza na viongozi wa kata, vijiji na wilaya za Simanjaro na Mwanga, zinazozunguka bwawa hilo, ili kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Meneja Miradi wa Shirika la Uasili wa Mazingira, Hosea Sanga alisema tayari wameanza kuwezesha wananchi wenye kipato cha chini wanaoishi maeneo yenye ukame, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaib Ndemanga na Mwenyekiti wa Watumiaji Maji Bonde la Pangani, Joseph Kajiru walisema kutokana na hali mbaya ya bwawa hilo, ni vema wananchi wakafuata sheria zilizowekwa za mazingira na maji ili kulinusuru kukauka.

Chanzo: Mtanzania


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa