Home » » Hatutozi viingilio kwa wanafunzi - TANAPA

Hatutozi viingilio kwa wanafunzi - TANAPA


na Grace Macha, Moshi
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limezitaka shule mbalimbali nchini kuacha kuwatoza wazazi fedha nyingi kwa ajili ya safari za watoto wao kutembelea hifadhi hizo kwani wanafunzi huingia bila kulipa viingilio.
Hayo yalisemwa juzi na Meneja Utalii wa TANAPA, Johnson Manase, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa Kanda ya Kaskazini kwenye warsha ya siku moja kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani.
Alisema kuwa TANAPA imekuwa ikishangazwa na kusikitishwa na hatua ya shule hizo kuwabebesha wazazi viwango vikubwa vya gharama wakati lengo la shirika ni kutowatoza wanafunzi viingilio ili kuwawezesha wengi zaidi kutembelea hifadhi hizo na kujifunza.
“TANAPA hatutozi wanafunzi viingilio kwenye malango yetu lakini kuna baadhi ya shule zinawatoza wazazi mpaka sh 70,000 kwa ajili ya kugharamia safari za watoto kutembelea hifadhi zetu, haiwezekani gharama za usafiri, malazi na chakula zikawa kubwa kiasi hicho,” alisema.
Pia meneja huyo, alikemea tabia mbaya ya “wadaka watalii” maarufu kama “flycatcher” waliozagaa kwenye maeneo mbalimbali ya kwenye mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwamba wanawasumbua pindi wanapopita kwenye maeneo wakijaribu kuwashawishi kuwaunganisha na kampuni za uwakala wa utalii.
Naye Katibu wa Chama cha Mawakala wa Utalii nchini (TATO), Cyril Akko, alisema kuwa ni vema mfumo wa ufundishaji wanafunzi mashuleni juu ya maliasili zilizopo nchini ukabadilishwa ili kuwajengea ari na nia ya kujifunza zaidi juu ya maliasili zilizopo nchini.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa