Home » » “Watoto wa Marais, Mawaziri Wasishike madaraka’

“Watoto wa Marais, Mawaziri Wasishike madaraka’


Daniel Mjema, Rombo
MKAZI wa Kijiji cha Mahida Nguduni wilayani Rombo, Patrick Kimaro amependekeza watoto wa marais na mawaziri wa sasa na wastaafu wasiteuliwe kugombea Urais wala kushika wadhifa wa Uwaziri.

Kimaro alitoa kauli hiyo jana katika eneo la Mamsera wakati akitoa maoni yake mbele ya Wajumbe wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya iliyokuwa chini ya Profesa Mwesiga Baregu.
“Hivi sasa dalili ya viongozi wakuu na mawaziri kutaka kurithishana uongozi na watoto wao, kama baba yako alishakuwa Rais au Waziri basi wewe mtoto usigombee tena Urais”alisema Kimaro.
Hata hivyo mchango wake huo ulionekana kutoeleweka vizuri, ambapo Profesa Baregu alimtaka afafanue kama pendekezo hilo linaishia tu kwa watoto wa Rais ama linaenda mbali zaidi ya hapo.
Kimaro alifafanua kuwa pendekezo lake hilo anataka liwabane pia watoto wa watu ambao walishashika wadhifa wa Urais na kwamba katiba imzuie Rais kuwateua kuingia katika baraza la mawaziri.
Pia alitaka mikataba inayoingiwa kati ya Serikali na wawekezaji iwe wazi na ichapishwe kwenye magazeti, akisema usiri unaofanywa na serikali katika mikataba ndio chanzo cha vitendo vya ufisadi.
Halikadhalika Kimaro ambaye ni mwalimu kitaaluma, alipendekeza katiba ijayo imuondolee Rais kinga ya kutoshitakiwa ili ashitakiwe anapotenda makosa kama inavyotokea kwa raia wengine.
Pendekezo hilo liliungwa mkono pia na Mkazi wa Mamsera Juu, Kamili Mariki huku mkazi wa eneo hilo pia Jacob Shirima yeye akipendekeza Rais wa aina hiyo apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa