Home » » SERIKALI YAFUNGA SHULE YA MARANGU HILLS KUTOKANA NA KUHATARISHA MAISHA YA WANAFUNZI

SERIKALI YAFUNGA SHULE YA MARANGU HILLS KUTOKANA NA KUHATARISHA MAISHA YA WANAFUNZI


Na Florah Temba, Moshi-Kilimanjaro Yetu

SERIKALI  wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro,imefunga kwa muda usiojulikana shule ya msingi Marangu Hills iliyopo kata ya Marangu mashariki wilayani humo, kutokana na kuhatarisha maisha ya wanafunzi na wananchi wanaoishi maeneo hayo kwa kuachilia maji taka kwenye mto.

Shule hiyo ya Marangu Hills Academy ambayo inamilikiwa na kanisa la Pentekoste ni ya mchepuo wa Kiingereza ambapo inachukua wanafunzi kuanzia madarasa ya awali na msingi na ni ya kutwa na bweni.

Shule hiyo inadaiwa kujengwa hadi kwenye kingo za mito na kuelekeza mfumo wa majitaka kwenye mto ulioko jirani na shule hiyo ambao unatumiwa na wananchi wengi jambo ambalo ni kinyume cha sheria za afya na mazingira na ni hatari kwa usalama wa afya zao.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mkuu wa wilaya ya moshi Dkt. Ibrahim Msengi, alisema alifika shuleni hapo bila kutoa taarifa na kukuta mifumo ya majitaka ikiwa imeelekezwa kwenye mto, hali ambayo ilimlazimu kutuma wataalamu wa afya kwenda kufanya uchunguzi katika shule hiyo na  mto huo na kukuta hali mbaya ambayo inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa.

Alisema mara baada ya wataalamu kutoa taarifa za hali mbaya ya uchafuzi wa mazingira na chanzo cha maji,alilazimika kwenda katika shule hiyo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya, pamoja na wataalamu wa afya na kuifunga  hadi watakapoboresha mfumo wa maji taka na kubomoa ukuta uliojengwa kwenye kingo za mto na kuacha mita 60 kama sheria inavyoelekeza.

“Ni kweli shule ya marangu Hills tumeifunga kwa muda usiojulikana, na hiyo ni kutokana na shule hiyo kutokuwa na mfumo wa maji taka hivyo wakati vyoo vimefurika wanachakachulia kwenye mto jambo ambalo ni hatari sana kwa wanafunzi na hata wananchi wanaoishi maeneo yale kwani maji ya mto ule yanatumiwa na wananchi wengi,na tumefanya vile ili kuepusha magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu”alisema Dkt.Msengi.

Dkt. Msengi alifafanua kuwa shule hiyo imejengwa hadi kwenye kingo za mito jambo ambalo ni kinyume cha sheria na kwamba mazingira yake si mazuri na wala hayaridhishi.

Kutokana na hali hiyo Dkt.Msengi aliwataka wazazi kujijengea tabia ya kukagua maeneo ambayo watoto wao wanasoma badala ya kuendelea kuwa bize na kazi zao na  kuridhika kwa matokeo na jina la shule  kwa madai kuwa zipo shule ambazo si nzuri na ni hatari kwa wanafunzi.

Katika hatua nyingine wilaya hiyo imelifunga soko la marangu  kutokana na kukithiri kwa uchafu na kosekana kwa vyoo vya uhakika,jambo ambalo ni hatari kwa afya za wananchi wa maeneo hayo.

Akizungumzia suala hilo Dkt. Msengi alisema wamefikia maamuzi hayo kutokana na soko hilo kuwa chafu na maji yanayotoka chooni kuelekezwa mtoni jambo ambalo ni hatari sana na linaweza likachangia mlipuko wa magonjwa.


“Soko la marangu nalo tumelifunga kwani soko lile ni chafu na pale pana vyoo lakini vyoo vile vinatiririsha maji yake mtoni,sasa tumeamua kulifunga hadi pale ambapo mazingira yatakuwa mazuri na vyoo vitajengwa”alisema.

Blogzamikoa

4 comments:

Unknown said...

Tatizo hilo limeshashughulikiwa na tunaomba habari hii itolewe sasa maana ni muda mrefu sasa umeshapita! Asante!

Unknown said...

Tatizo hilo limeshashughulikiwa na tunaomba habari hii itolewe sasa maana ni muda mrefu sasa umeshapita! Asante!

Unknown said...

Tatizo hilo limeshashughulikiwa na tunaomba habari hii itolewe sasa maana ni muda mrefu sasa umeshapita! Asante!

Unknown said...

Hilo tatizolishatatuliwa litolewe!

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa