Home » » MKE WA MTOTO WA DC ATEKWA NA KUPORWA

MKE WA MTOTO WA DC ATEKWA NA KUPORWA


na Charles Ndagulla, Moshi

WIMBI la matapeli wanaotumia vitambulisho vya maofisa Usalama wa Taifa na majeshi mengine, limechukua sura mpya baada ya watu takriban wanane, akiwamo mwanamke mmoja, kumtapeli mke wa mtoto wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi, jijini Dar es Salaam.

Matapeli hao inadaiwa walisafiri kutoka Dar es Salaam hadi mjini Moshi na kumteka mke huyo na kumsafirisha hadi jijini humo na kisha kumpora dola za Marekani 11,000 (zaidi ya sh milioni 15).

Tukio hilo limetokea Oktoba 11, mwaka huu, eneo la Soweto mjini hapa ambako matapeli hao wakitumia gari aina ya Toyota RAV4, walifika nyumbani kwa mtoto wa DC huyo, Jerome Tingisi na kujitambulisha kama maofisa wa polisi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba.

Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, watu hao walimkamata mke wa Jerome wakimtuhumu kujihusisha na biashara ya dawa ya kulevya na kumtaka aongozane nao hadi Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ndiko jalada la uchunguzi lililokofunguliwa.

Mtoa taarifa aliyeomba jina lake lisitajwe, alisema watu hao walimchukua mke huyo na kumsafrisha hadi Dar es Salaam na baadaye walitumia simu yake kuwasiliana na mume wake wakimtaka awape sh milioni mbili huku wakitishia kumuua kama matakwa yao yasingetekelezwa.

Hata hivyo, mtoa taarifa wetu alisema kuwa watu hao waliamua kumtelekeza katika eneo la Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam huku wakiondoka na ‘breafcase’ ikiwa na kiasi hicho cha fedha.

Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, baada ya matapeli hao kumteka mwanamke huyo, Hawa Jerome, walimchukua kwa maelezo kuwa wanampeleka Kituo Kikuu cha Polisi mjini hapa lakini hawakufanya hivyo.

Jerome alithibitisha jana kutekwa kwa mkewe na licha ya kutaka habari hizo zisichapishwe, aliongeza kuwa watekaji hao walitumia bastola, pingu tatu na radio ya mawasiliano ya polisi kufanikisha utekaji huo.

Akizungumza na gazeti hili, Jerome alisema kuwa kwa sasa wanawasaka watuhumiwa kwa ushirikiano na maofisa wa polisi jijini Dar es Salaam na Moshi ili kuwatia mbaroni, huku akimtaja mmoja wao kuwa anaitwa Deo.

Alisema Deo anayeishi eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, ndiye aliyeongoza wenzake kumteka mkewe na amekuwa akivichafua vyombo vya dola kwa kujipachika wadhifa wa ofisa Usalama wa Taifa, akiwa na vitambulisho vya idara hiyo.

Hata hivyo, tukio hilo limekumbwa na habari za mkorogano, kwani taarifa nyingine zinadai kuwa mwanamke huyo alisafirishwa hadi Dar es Salaam na kuwekwa kwenye hoteli moja ambako aliahidi kuwapatia matapeli hao sh milioni 100, lakini baada ya kubaini si maofisa wa polisi aliwasiliana na jamaa yake aliyetajwa kwa jina moja la White.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa