Home » » Serikali yaahidi kumfukuza mkandarasi

Serikali yaahidi kumfukuza mkandarasi

SERIKALI imeahidi kumfukuza mkandarasi anayejenga barabara ya Mkumbara hadi Same, endapo hatabadilika kutokana na utekelezaji wake katika mradi huo. Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Gerson Lwenge, aliyasema hayo wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 96.

Alisema mkandarasi huyo, ameshatumia zaidi ya nusu ya muda, lakini utekelezaji wake ni asilimia 20.

Alisema mkandasi huyo kutoka kampuni ya Dott Services ya nchini Uganda, ameonekana kutekeleza mradi huo kwa taratibu sana, wakati anatakiwa kukamilisha Agosti 4 mwaka 2014.

“Serikali tutamfukuza mkandarasi huyu kama hatabadilika na kumaliza kazi hii kwa muda uliopangwa, kwani hadi sasa ameshatekeleza kwa asilimia 20 tu wakati ashatumia muda zaidi ya nusu,” alisema.

Alisema serikali haitakuwa tayari kumuongezea muda endapo muda wake utakwisha kutokana na kwamba ameonekana kuwa na vifaa vingi, lakini tatizo ni kutokuwa na mpangilio mzuri.

Akizungumza, Meneja Wakala wa Barabara Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Marwa Rubirya, alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa kazi, ikiwemo kutotolewa kwa wakati fedha za matengenezo ya barabara.

Alisema changamoto nyingine ni kutengwa kwa fedha kidogo za miradi ya maendeleo, hali ambayo inasababisha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo kutoanza kama ilivyopangwa.

“Kutokamilika kwa wakati kwa miradi ya ahadi ya serikali, kutokana na madeni makubwa yanayodaiwa na makandarasi, nayo ni changamoto kubwa, kwani hali hii inasababisha kuongezeka kwa gharama za miradi na kuchelewa kukamilika kwa miradi,” alisema.
Chanzo: Rai

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa