|
MKURUGENZI Mkuu wa Hifadhi za Taifa nchini, (TANAPA), Allan
Kijazi, amewataka wapagazi wanaosaidia kubeba mizigo ya watalii kwenye
Mlima Kilimanjaro kuhakikisha wanatunza mazingira ya mlima huo kwani
ukiharibika na wao wataathirika kwa kukosa ajira.
Aidha, alisema atawasiliana na wadau wa utalii ili kuona namna ya
kuboresha utendaji wao kwa kuwatafutia ziara ya mafunzo kwenye moja ya
nchi zenye milima mirefu.
Aliyasema hayo jana wakati akifungua kongamano la kwanza la Chama
Cha Wapagazi nchini (TPO) lililofanyika kwenye ukumbi wa YMCA ambalo
lilikuwa likijadili changamoto wanazokabiliana nazo na namna ya
kuzitatua.
Kijazi alisema kuwa kwenye kongamano lao hilo mbali ya kujadili
changamoto zinazowakabili ni vema wakaangalia namna ya kuutunza mlima
huo ambao unawapatia ajira.
“Kuna malalamiko yanakuja kuwa wakati mwingine nyie mnaacha taka
huko mlimani kwa kushindwa kuzikusanya vizuri, ni vema mkautunza mlima
huu kwani ukipoteza sifa na hadhi yake wageni wataacha kuja na nyie
mtakosa ajira,” alisisitiza mkurugenzi mkuu huyo wa Tanapa.
Aliwataka viongozi wa TPO kujenga mfumo wa kufuatilia mienendo ya
wanachama wao ili kuona kama wanafuata taratibu na maadili
waliyojiwekea, kwani kuna wakati yanaibuka malalamiko kuwa kuna baadhi
ya wapagazi si waaminifu na wengine hawazingatii uvaaji sahihi, jambo
linalohatarisha usalama wa afya zao.
Kijazi alisema kuwa anaangalia uwezekano wa kukutana na wadau wa
utalii wanaoendesha shughuli kwenye mlima huo wakiwemo Chama cha
Waongoza Watalii kwenye mlima huo, KIATO, na Wizara ya Maliasili na
Utalii ili waweze kuona namna sheria zilizowekwa hasa kwenye udhibiti wa
uzito wa mizigo zitakavyosimamiwa kwa ukaribu zaidi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri, TPO, Richard Kessy,
alisema changamoto kubwa zinazowakabili wapagazi ni kampuni za uwakala
wa utalii kubebeshwa mizigo mizito zaidi ya kiwango kilichowekwa na
Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) ambacho ni kilogramu 20.
“Wapagazi wakiwa huko mlimani kuna wengine wanapewa chakula mara
moja kwa siku, wengine wanapewa mara mbili lakini kidogo sana
ukinganisha na kazi ngumu ya kubeba mizigo yao na ya watalii
wanayoifanya,” alisema Kessy.
Naye Mwenyekiti wa TPO, Philip Mbise, alisema kuwa wana wanachama
2,820, ambapo kongamano hilo la siku moja limehudhuriwa na wapagazi 250
kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment