Home »
» KMCM kinara mlipakodi Kilimanjaro
KMCM kinara mlipakodi Kilimanjaro
|
|
HOSPITALI ya Rufaa ya KCMC kwa mara ya tatu mfululizo
imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika kundi la walipakodi wakubwa
wa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kutunukiwa cheti cha ubora na Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA).
KCMC imeshika nafasi hiyo baada ya kushindanishwa na makampuni na
taasisi mbalimbali katika eneo la walipakodi wakubwa wakati wa
maadhimisho ya saba ya Siku ya Mlipakodi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti cha ubora, Mkurugenzi wa
hospitali hiyo, Profesa Moshi Ntabaye, alisema uongozi wao umekuwa
ukifanya kazi kwa karibu na serikali kwa kufuata taratibu na miongozo
iliyowekwa.
“Sisi katika kujipangia kwetu kazi, tumeona kwamba ni vyema kufuata
miongozo ya serikali, mojawapo likiwa ni hili la kulipa kodi na tumeona
tuwe wa mfano kulipa kodi zote zinazohitajika, na pili kama taasisi ya
kanisa ni wajibu wetu kufundisha kwa mfano,” alisema Ntabaye.
Alisema siri ya mafanikio ya ushindi wa hospitali hiyo pia ni uelewa
kwa wafanyakazi na taasisi ya KCMC kutokana na ushiriki wao katika
kulipa kodi, hasa ile inayotokana na makato katika mishahara yao pamoja
na mapato mengine yanayopatikana katika hospitali hiyo.
Ntabaye alisema wagonjwa wengi wanachangia huduma ya afya katika
hospitali hiyo, hivyo ni wajibu wao kama viongozi kuona kiasi cha
michango ya wananchi hao kinarudishwa kwao kwa njia ya kodi ili iweze
kutumika katika kuboresha maeneo mengine.
Alisema KCMC imekuwa ikichangia si chini ya sh milioni 150 kama kodi
na ndiyo sababu imekuwa ikitunukiwa tuzo hiyo kwa mwaka wa tatu
mfululizo.
Meneja wa TRA, Patience Minga, alisema hospitali ya KCMC kuibuka
mshindi wa jumla kwa walipakodi wakubwa, inadhihirisha kuwa huduma
zitolewazo zinajali wateja wake.
Minga alisema TRA kila mwaka imekuwa ikishindanisha makampuni na
taasisi mbalimbali katika tuzo hizo, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi
katika suala zima la ulipaji kodi, ikiwa ni pamoja na kuleta hamasa ya
umuhimu wa kulipa kodi.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment