WATAALAMU wa usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori kutoka nchi zaidi
ya 20 duniani wamekutana mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kujadili
matumizi ya teknolojia mpya ya kubaini majangili.
Hatua hiyo inakuja wakati huu ambao baadhi ya wabunge wamekuwa
wakiituhumu serikali kuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua dhidi ya
viongozi wake wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu.
Teknolojia hiyo ya kisayansi iliyoibuliwa nchini Marekani ijulikanayo
kama Forensic Science Laboratory imekuja wakati sakata la ujangili
likiwagawa wabunge na baadhi ya mawaziri wanaodaiwa kujihusisha na
biashara hiyo.
Licha ya kuingizwa katika mitaala ya vyuo vya usimamizi na uhifadhi wa
wanyamapori nchini, itatumiwa na vikosi vya operesheni za ujangili
vinavyojumuisha maofisa wa Usalama wa Taifa, Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), askari wa wanyamapori, polisi na wataalamu wa vyuo vya
wanyamapori.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya usimamizi, uhifadhi wa
wanyamapori na utalii yanayoendelea katika Chuo cha Mweka, Mkuu wa Chuo
cha Wanyamapori nchini Kenya, Prof. George Otiang’a, alisema teknolojia
hiyo imefanikiwa kutokomeza ujangili kwa kiasi kikubwa nchini Marekani
na kwamba katika Bara la Afrika nchi ya Afrika Kusini ndiyo nchi pekee
iliyoanza kuitumia.
Alisema kwa sasa wameanza mashauriano kuhusu teknolojia ya kisayansi
ambayo inawawezesha askari na wataalamu wa masuala hayo kuwagundua
majangili kupitia taarifa za vinasaba (DNA) kwa kupima damu ya mnyama.
Pia watapima alama za nyayo za majangili pamoja na alama za vidole vya majangili katika mwili wa mnyama aliyeuawa.
“Mbinu hiyo itaondoa utata wa kuwabaini wahusika kupitia taarifa za
DNA, Kenya na Tanzania ndiyo tupo kwenye mchakato wa kuingiza aina hiyo
ya utambuzi wa kisayansi kwenye mitaala ya vyuo vya usimamizi na
uhifadhi wa wanyamapori ili kukabiliana na wimbi hili la
ujangili wa tembo na faru Afrika ya Mashariki,” alisema.
Kwa mujibu wa Otiang’a, hali ni mbaya na kila nchi imekuwa ikijadili
na Tanzania inaangalia uwezekano wa kuzishauri serikali za mataifa
husika, ingawa teknolojia hiyo ni gharama kubwa kuiendesha.
Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na hatua hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha
Usimamizi na Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika (Mweka), Dk. Freddy
Manonge, alisema hivi sasa Tanzania iko kwenye mchakato wa kuandaa
mtaala unaotumia teknolojia ya kutambua wahalifu wa ujangili katika
hifadhi zote zilizopo hapa nchini ili kuondoa kigugumizi cha kukwepa
kuwashughulikia wahusika wa ujangili ambao wameiweka rehani rasilimali
hiyo adimu.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Dk. Alex Kissingo, alisema
tatizo la ujangili wa wanyapori nchini ni kubwa na kwamba wengi ambao
wamekuwa wakikamatwa kwa matukio hayo ni watumishi wa serikali na
hifadhi za wanyamapori.
Naye Dk. David Manyanza ambaye aliwahi kuwa mkuu wa chuo hicho,
alisema vita dhidi ya ujangili inaonekana kuwa ngumu kutokana na usiri
unaotumika katika biashara hiyo pamoja na kuwapo kwa mkono wa watu
mashuhuri wakiwamo viongozi wa juu ndani ya serikali.
Alisema ikiwa kutakuwa na utashi wa dhati katika mapambano haya kutoka
kwa wananchi wenyewe, serikali pamoja na wafanyabiashara, tatizo la
ujangili linaweza kumalizika
CHANZO;TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment