JIBU LA SWALI LA MBUNGE Rombo
SERIKALI imehojiwa kama haioni utaratibu Bodi ya Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) kuzuia uendelezaji wa miradi ya shirika hilo
inayoingia mkataba na wawekezaji wa ndani kupitia PPP na kudai ni
lazima ipitiwe upya ili kuruhusu NHC kupewa hisa za ziada kabla ya
mradi kukamilika, kinyume cha mikataba ya awali ni kukatisha tamaa
wawekezaji wa ndani na kuzuia jitihada za serikali kuhamasisha miradi ya
PPP.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa na Mbunge wa Rombo, Joseph
Selasini (CHADEMA), ambapo pia alitaka kujua kama serikali haioni
kwamba shauri la mwekezaji kuingia gharama zote kama upembuzi yakinifu,
usanifu wa majengo na gharama za ubomoaji wa majengo ya zamani
likiende mahakamani linaweza kuigharimu serikali fedha nyingi za walipa
kodi kama fidia kwa usumbufu waliousababishiwa wawekezaji.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA),
alitaka kujua kama serikali iko tayari kutembelea eneo la Ubungo
kutatua mgogoro uliopo baina ya wananchi wanaoishi katika nyumba za NHC
na menejimenti ya shirika hilo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Goodlucky Olemedeye, alisema wizara yake inakiri kupokea
malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wanaopinga miradi ya ubia ilikuwa
ikiendeshwa baina ya shirika hilo na wawekezaji wa sekta binafsi.
Alisema msingi wa malalamiko hayo ni kiwango cha uwazi katika kuingia
mikataba, usimamizi wa miradi na masilahi madogo kwa upande wa NHC.
“Kwa mfano, mikataba iliyo mingi ilikuwa inatoa asilimia 25 ya hisa
zote za mradi kwa NHC na inayobaki inachukuliwa na wawekezaji,” alisema
naibu waziri.
Alifafanua kuwa kufuatia malalamiko hayo mwaka 2009 serikali
ilisimamisha zoezi la NHC kuingia mikataba mipya ya miradi ya ubia.
Menejimenti na bodi mpya ilipoanza kazi Machi 2010, serikali iliagiza
kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba ya miradi ya ubia kwa
lengo la kuiboresha na hususan kubainisha taratibu zilizofuatwa hadi
kufikia mikataba ya miradi hiyo na kuyafanyia kazi malalamiko ya
wananchi ipasavyo.
Akijibu swali la Mnyika, naibu waziri huyo alisema yuko tayari kufika
katika eneo hilo la Ubungo akiwa na menejimenti yake ili waweze
kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
chanzo;tanzania daima
0 comments:
Post a Comment