Home » » Wafanyabiashara Moshi wamtwisha zigo Ndesamburo

Wafanyabiashara Moshi wamtwisha zigo Ndesamburo

Philemon Ndesamburo
Wafanyabiashara wa mji wa Moshi, wamemuomba mbunge wa jimbo hilo, Philemon Ndesamburo (Chadema), wakimtaka awasaidie kupeleka haraka hoja binafsi katika mkutano ujao wa Bunge kupinga matumizi ya mashine za kielekroniki (EFD).
Wanataka wabunge watoe uamuzi ili serikali ifanye maboresho katika mashine hizo au kupunguza gharama zake kwa madai kuwa wafanyabiashara wadogo wameshindwa kumudu gharama na kusababisha misuguano kati yao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo inasisitiza ukomo wa kununua mashine hizo ilikuwa ni Desemba 31, mwaka huu.

Walitoa ombi hilo kwa Ndesamburo  alipokwenda kuzungumza na wakazi wa Kata ya Kiboroloni ambao walimpoteza Diwani wao na Naibu Meya wa Manispaa ya Moshi, Vicent Rimoy wiki mbili zilizopita.

Freddy Moshi alisema wakazi wa Manispaa hawana imani na mashine za kielekroniki ambazo zinatumiwa kukusanya kodi kwa kuwa zina harufu ya kifisadi.

Kanael Meena alimwomba mbunge huyo kubeba jukumu la kukiharakisha chama chake kupeleka hoja binafsi bungeni kupinga matumizi ya mashine hizo akisema kuwa zinawanyonya wafanyabiashara wadogo na wananchi wenye kipato cha chini na kwamba ili kuepusha misuguano kati ya serikali na wafanyabiashara hana budi kujitwisha zigo hilo.

“Tumewaona wenzetu Dar es Salaam na mikoa mingine ya Mbeya na Arusha namna ambavyo wanalalamikia mashine za EFD  hadi wakayafunga maduka yao kushinikiza serikali ilitazame upya suala hilo.

Hatutaki Moshi nao waanze huo mshikemshike, ndiyo maana tunakutuma,” alisema Omega Munuo.

Akijibu ombi hilo, Ndesamburo alisema atawasilina na uongozi wa chama chake ili kujua kwamba mchakato wa hoja hiyo kupelekwa bungeni kama kilivyoahidi na kuwataka  kuwa wavumilivu wakati akishughulikia wazo hilo.

Rai hiyo ya wafanyabiashara wa Moshi inaungwa mkono na Mwenyekiti wa Chama cha Wenye Viwanda, Biashara na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Shirima, ambaye alimtaka  Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa kuwaongezea muda hadi Machi mwakani.
 
CHANZO: NIPASHE



0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa