Home » » Wahabeshi 93 mbaroni kwa kuingia nchini kinyemela

Wahabeshi 93 mbaroni kwa kuingia nchini kinyemela

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro,Robert Boaz
 
Raia  93 wa Ethiopia, wametiwa mbaroni kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Kilimanjaro kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
Katika tukio la kwanza, Waethiopia 56 walikamatwa katika kijiji cha Jiungeni kata ya Ruvu Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana wakiwa katika gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 188 AYU mali ya Elimo Trans.

Alisema gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Daniel Mfinanga, mkazi wa Himo,  lilikamatwa na kupelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha mjini Moshi.

 “Mbali ya raia hao wa kigeni, alisema pia Watanzania watatu akiwamo dereva wa Fuso, walitiwa mbaroni kwa tuhuma za kuwasafirisha wahamiaji hao haramu.

Kamanda Boaz alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwafichua wahamiaji haramu wanaoingia nchini kinyume cha sheria pamoja na wanaojihusisha na biashara hiyo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Katika tukio la pili, Waethiopia 37 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kuingia nchini bila kibali.

Kaimu Kamanda wa Polisi, John Laswai, alisema Waethiopia hao walikamatwa juzi saa 12:00 jioni katika eneo la Kidai tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa wakitokea jijini Dar es Salaama wakielekea uelekeo wa mkoani Iringa.

Alisema walikamatwa wakiwa kwenye malori mawili tofauti yenye namba za usajili T543 ACK likiendeshwa na Samson Karanga (25) na Laizer Samuel (25), wakazi wa Arusha na lenye namba T363 AMK lililokuwa likiendeshwa na Massawe Kennedy (38), pia mkazi wa Arusha.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa