Home » » DAWA ZA KULEVYA ZAITESA KILIMANJARO

DAWA ZA KULEVYA ZAITESA KILIMANJARO

MKOA wa Kilimanjaro umetajwa kuongoza kwa matukio ya dawa za kulevya, katika kipindi cha mwaka jana, huku mirungi na bangi vikionekana kuathiri vijana wengi, ambao ndio nguvu kazi ya taifa.
Taarifa kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa mwaka 2013, inaonesha jumla ya kilo 5,909.557 za dawa za kulevya zilikamatwa katika maeneo mbalimbali, zikilinganishwa na mwaka 2012, ambapo zilikamatwa kilo 1,799.617.

Taarifa hizo zinaonesha kuwa tofauti na ilivyokuwa mwaka 2012, jumla ya kilo 3,986.276 za mirungi, zilinaswa mkoani humo, kiwango ambacho ni kikubwa ukilinganisha na kilo 1183.826 zilizokamatwa mwaka juzi wa 2012.

Aidha taarifa hizo pia zinaonesha kuwa katika kipindi hicho, kumekuwa na idadi kubwa ya wavuta bangi, ambayo ni zaidi ya kilo 1,908.776 zilizokamatwa mkoani humo katika maeneo mbalimbali, kiwango ambacho ni kikubwa kikilinganishwa na kilo 601 zilizokamatwa mwaka 2012.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, Robert Boaz alisema katika kipindi cha mwaka 2013, watuhumiwa 759, walikamatwa na kufikishwa mahakamani kuhusiana na matukio ya kusafirisha au kukutwa na dawa hizo.

Katika matukio hayo kati ya Novemba na Desemba mwaka jana, jumla ya watuhumiwa wanne wa kigeni walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa (KIA), kutokana na operesheni maalumu ya polisi wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine.

Chanzo;Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa