MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi imetoa zuio la kutouzwa jengo la
Ushirika wa Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii lililopo chini
ya mradi wa shamba la miti la Rongai wilayani Rombo.
Jengo hilo ilikuwa liuzwe kupitia Kampuni ya udalali ya Mariperanto,
ili kufidia deni wanalodaiwa wanaushirika hao na mmoja wa wanaushirika,
Manase Seleman.
Chimbuko la kuuzwa kwa jengo hilo linatokana na wanaushirika wenzake
kukiuka makubaliano ya kumlipa deni lake kupitia makato ya makusanyo ya
mapato katika mradi wa basi baada ya kutumia fedha zake kulifanyika
matengenezo.
Inadaiwa siku mbili baada ya kulifanyia matengenezo basi hilo na
kuingia barabarani mwaka 1987, mwanaushirika huyo ambaye alikuwa ni
dereva aligeuziwa kibao na wanaushirika wenzake na kukamatwa na polisi
kwa tuhuma za wizi wa basi hilo.
Manase anadai wanaushirika wenzake walimtungia kesi ya uongo kwa
lengo la kumdhulumu haki yake na ndipo alipoamua kufungua kesi Mahakama
Kuu mjini Arusha mwaka 1987 na tangu mwaka huo ameshinda mara nne
zikiwamo rufaa tatu.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Meneja mradi
shamba la miti Rongai, Julius Mkumbo, alisema jengo hilo ni mali ya
serikali na si mali ya wanaushirika.
Alisema wafanyakazi hao waliamua kuunda umoja wao kwa lengo la
kujiongezea kipato na kulitumia kuendeshea shughuli zao, hivyo
mwanaushirika huyo hawezi kulihusisha na madai anayowadai wanaushika
wenzake.
Kutokana na hatua ya mahakama kutoa ruhusa ya kuuzwa kwa jengo hilo,
meneja huyo alisema wamewasilisha pingamizi mahakamani kupinga kuuzwa
kwa jengo hilo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment