WAZIRI
wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, ameikataa taarifa ya hali ya utoaji
wa huduma ya maji kwa Mkoa wa Kilimanjaro iliyosomwa na Mhandisi wa Maji
wa mkoa huo, Immaculate Rafael, kutokana na kujaa makosa.
Waziri Maghembe alikuwa akipokea taarifa ya hali ya huduma ya maji
kwa mkoa huo pamoja na kufanya ziara ya kuzindua upatikanaji wa maji
katika Kata ya Kiboriloni na Ngambo maeneo ambayo yalikuwa yakikabiliwa
na tatizo la ukosefu wa huduma hiyo kwa kipindi kirefu.
Taarifa hiyo ilishindwa kuonyesha takwimu za kila wilaya na idadi ya
watu wanaopata maji na kwa asilimia gani, hatua iliyomlazimu Profesa
Maghembe kusema kuwa njia iliyotumika kukokotoa takwimu hizo si sahihi.
“Nimesimama kueleza kuwa taarifa ya huduma niliyosomewa na mhandisi
nilikuwa naifuatilia na kugundua kuwa ina makosa kwenye takwimu zilizopo
na makosa hayo yametokana na njia iliyotumika kukokotolea takwimu hizo
ambazo si sahihi, ” alisema.
Alisema kuwa uandaaji wa takwimu hizo ulikuwa na kasoro mbili; moja
ikiwa ni jinsi ya kukokotoa pamoja na kuunganisha idadi ya watu
wanaopatiwa maji maeneo ya mjini na maeneo ya vijijjni, jambo ambalo si
sahihi.
Maghembe alisema kuwa katika kutafuta wastani wa wananchi wanaopata
huduma ya maji lazima takwimu zionyeshe uhalisia wa watu wanaopata maji
kulingana na wilaya na maeneo husika.
“Katika kutafuta wastani wa wilaya ambazo watu wake wanapatiwa maji
huwezi kuchukua Wilaya ya Siha ambayo upatikanaji wake wa maji ni
asilimia 80, Mwanga asilimia 68 na Moshi asilimia 75 ukajumlisha na
kupata uhalisia wa watu wanaopata hiyo huduma,” alisema.
Hata hivyo alimtaka mhandisi huyo kusahihisha taarifa hiyo ili kupata
takwimu halisi zenye kuonyesha wastani wa watu wanaopatiwa huduma hiyo.
Akitolea mfano Wilaya ya Rombo ambapo kuna mabonde na makorongo,
alisema ni vema kuweka utaratibu utakaowawezesha kupata hesabu sahihi za
wananchi wanaopata huduma hiyo.
Alisema katika lengo la taifa la upatikanaji wa maji na malengo la
milenia ya serikali ni kuhakikisha kuwa huduma ya maji mijini
inapatikana kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2015.
ChanzoTanzania Daima
0 comments:
Post a Comment