WAGONJWA wanaotibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, watumishi
na wageni wanaowauguza wagonjwa, afya zao zipo hatarini kutokana na
kukumbwa na magonjwa ya mlipuko na maji wanayotumia katika hospitali
hiyo kudaiwa si safi na salama.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini taarifa za maji
yanayotumiwa kwenye hospitali hiyo kudaiwa kuwa na dalili za uchafu
(contaminated), iliyoibuliwa na mmoja wa madaktari (jina tunalo) kwenye
kikao kilichokaa Januari 8, mwaka huu baada ya kuyafanyia maji hayo
utafiti.
Awali Hospitali ya Rufaa ya KCMC ilikuwa ikitumia maji ya kwenye
tanki ambayo yalikuwa yakiwekwa dawa, lakini matumizi ya maji
yalipokuwa mengi ililazimu kuyafungulia maji hayo kuingia kwenye
mzunguko moja kwa moja kutoka kwenye visima.
Mkurugenzi wa huduma wa hospitali hiyo, Profesa Raimos Olomi, ambaye
pia alikuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Hospitali, alikiri kuwepo
kwa tatizo hilo huku akisema walishafanya utafiti wa awali lakini
wanasubiri matokeo kutoka mamlaka ya maji.
“Ni kweli tatizo hilo lipo maji kudaiwa ni dalili za uchafu
(contaminated) lakini tunasubiri majibu ya mamlaka na tatizo si kubwa
kwa sababu kuna maeneo mengine maji ni safi na salama lakini maeneo
mengine yameonekana kuwa na tatizo,” alisema.
Taarifa za ndani zilieleza kuwa huenda tatizo hilo la maji kuwa
machafu linaweza likawa limesababishwa na moja ya visima vinavyotumiwa
na hospitali hiyo kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu.
Watumishi waliozungumza na Tanzania Daima walisema uongozi
haujachukua hatua za haraka tangu tatizo hilo la maji lilipogundulika,
hali ambayo inashusha hadhi ya hospitali hiyo inayotegemewa nchi nzima
pamoja na nje ya nchi.
Kwa upande wa kisima kuwa ndiyo sababu ya maji hayo kuwa machafu
kutokana na kutofanyiwa usafi, alisema kama ingekuwa chanzo cha maji
wanayotumia ndiyo inapelekea maji hayo kuwa machafu basi maeneo yote
maji yangeonekana machafu, hivyo si tatizo linalotokana na chanzo.
Hata hivyo kutokana na tatizo hilo hospitali hiyo imetoa tahadhari
ambapo kuna wagonjwa, watumishi na wageni wengine wanaowaangalia
wagonjwa kulazimika kununua maji ya chupa madukani ili kuweza kuepukana
na hali hiyo.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment