Home » » Rombo ‘wawatunishia misuli’ maofisa H/shauri

Rombo ‘wawatunishia misuli’ maofisa H/shauri

Watumishi wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo juzi walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuwekwa chini ya ulinzi wa wananchi wenye hasira, walipokwenda kutwaa ardhi ya vikongwe wawili.
Siku tatu kabla ya kufika eneo hilo, maofisa hao inadaiwa walifika tena na kuwapa siku tatu za kukubali kupokea fidia ama wanyang’anywe kwa madai Rais analihitaji eneo hilo kujenga Ikulu.
Mmoja wa wananchi hao, Living Njau ambaye ni mwanafamilia ya kikongwe James Maingi, alisema wao walipewa siku tatu hadi kufikia hiyo juzi wawe wamekubali kuhama na kupokea fidia.
“Niliwaomba wanipe angalau wiki mbili nijadiliane na familia wakakataa nikawaomba wiki moja wakakataa wakasema Serikali inalitaka kwa haraka eneo hili na muda umepita,” alisema.
Mmoja wa familia ya Christosia Kombe alisema maofisa hao waliwaambia Rais analitaka eneo hilo kwa ajili ya kujenga Ikulu na kama watagoma kulitoa, Rais angewanyang’anya bila kuwalipa fidia.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alikana Serikali kuwa na mpango wa kujenga Ikulu eneo hilo na kuagiza vyombo vya dola ikiwamo Polisi kuchunguza suala hilo.
Kutokana na maagizo hayo ya mkuu wa mkoa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alituma polisi wakiwa katika Landrover mbili saa 11:30 jioni na kuwakamata maofisa hao.
Maofisa hao na vyeo vyao vikiwa kwenye mabano ni Arbogust Mhuba (Ofisa Ardhi), Hilaria Ephrem (Fundi Sanifu), Ronadl Amos (mpima ramani) na Andrew Gregory (Mwanasheria wa Halmashauri).
Pia miongoni mwa waliokamatwa ni mwenyekiti wa kijiji hicho, Januari Lyimo aliyekuwa amefuatana na maofisa hao ambao baadae waliachiwa kwa dhamana saa 5:00 usiku katika kituo cha Holili.
Maofisa hao walikwenda katika Kijiji cha Holili kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya Jumapili saa 8:00 mchana wakiwa na gari binafsi aina ya Toyota Surf namba T.406 BXN rangi ya bluu.
Hata hivyo, Mhuba akihojiwa na wananchi katika eneo hilo huku akirekodiwa, alikiri kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya hakuwa na taarifa ya kazi hiyo.
Alipoulizwa nani atawarejeshea mafuta waliyotumia kufika katika kijiji hicho kwa kutumia gari binafsi wakati magari ya Serikali yapo mengi, alisema mkurugenzi atawarudishia fedha hizo.
Baada ya kubanwa sana, Mhuba alijitetea walikwenda kwa vikongwe hao kuzungumza nao tu ili wakubali kupokea fidia kwa kuwa kijiji hicho kinatakiwa kiingizwe kuwa mji mdogo Holili.
Diwani wa eneo hilo, Onesmo Myombo, alisema mpango wa kuliingiza eneo hilo mji mdogo wa Holili ulisitishwa Septemba 2012 katika mkutano wa hadhara baada ya wananchi kugoma.
Hata hivyo, alisema alishangaa kuona Ijumaa akipigiwa simu na mwenyekiti wa kijiji, Januari Lyimo akimweleza kuwapo ujio wa maofisa ardhi kwa jambo ambalo lilisitishwa tangu mwaka 2012.
“Nilimwambia hilo jambo waliache litawaletea matatizo kwa sababu lilisitishwa kwenye mkutano wa wanakijiji wote na kama ni kulianzisha tena ni lazima uitishwe mkutano wa kijiji”alisema.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Anthony Tesha alishangaa watumishi hao kufanya kazi kienyeji wakati taratibu za kutwaa ardhi ya mtu zinafahamika na halazimishwi.
Kamanda wa Polisi, Robert Boaz alisema polisi wamefungua jalada la uchunguzi ili kuona kama kuna vitendo vya kijinai vimefanywa na jalada hilo limehamishiwa mkoani kutoka Kituo cha Holili.
Chanzo;MMwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa