Home » » Uhamiaji watuhumiwa kuhujumu mgombea Chadema

Uhamiaji watuhumiwa kuhujumu mgombea Chadema

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
 
Mgombea udiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mdogo kata ya Kiboriloni, Manispaa ya Moshi, Frank Kagoma, ameitwa na Idara ya Uhamiaji mjini hapa kwenda kuthibitisha uhalali wa uraia wake ambao unatiliwa shaka.
Hata hivyo, Kagoma ambaye anawania kiti hicho akichuana vikali na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Willy Tulli na mgombea wa UDP, Adon Mzava, amesema hayuko tayari kuitikia wito huo kutokana na kushauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kutokwenda hadi hapo chama kitakapotoa maelekezo.

“Nimeitwa na Ofisa Uhamiaji (bila kumtaja jina), akaniambia eti mimi siyo raia, nikamwambia mimi nimezaliwa Moshi na nimekulia Moshi iweje leo mimi si raia.

Najua lengo lao ni kutaka kunibugudhi kwa sababu hii si mara ya kwanza kuulizwa hili suala ... mwaka 2005 wakati nagombea nafasi ya uenyekiti wa mtaa, niliwapatia vielelezo,” alisema Kagoma katika mkutano wa hadhara wa kampeni Jumamosi iliyopita.
Alisema: “Hivi karibuni wakati kampeni zinaanza pia wakaja nikawapatia vielelezo vyote, lakini licha ya kuwapatia vielelezo, bado wananitaka niende tu.”

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema katika mkutano huo kuwa baadhi ya maofisa uhamiaji wanataka kumdhoofisha mgombea huyo katika uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani wakati maadili ya uchaguzi hayasemi hivyo.

“Sikiliza nakupatia ushauri wa bure, siku nyingine itabidi nikutoze gharama za uwakili, huyo ofisa uhamiaji akija, sijui ni wa wilaya, mkoa au kanda, mwambie mwanasheria wangu ni Tundu Lissu,” alisema Lissu katika mkutano huo.

Lissu alisema mwaka 2010 Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitunga sheria inayoitwa kanuni za maadili ya uchaguzi na kwamba sehemu ya maadili ya uchaguzi inazungumzia maadili ya watumishi wa serikali kuhusiana na uchaguzi.

Alisema sehemu ya maadili inasema itakuwa marufuku kwa vyombo vya serikali au vyombo vya usalama kusumbua wagombea au vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, hivyo anachokifanya ofisa uhamiaji anakiuka maadili ya uchaguzi yaliyotungwa na NEC.

Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Yohanes Msumile, alipoulizwa na NIPASHE kuhusiana na suala hilo, alisema:

“Mimi ndiyo kwanza naingia ofisini leo, nilikuwa Mwanza kikazi kwa hiyo bado sijapata taarifa za madai hayo, lakini nitalifuatilia kwa umakini mkubwa.

Kama yapo madai hayo tutafanya uchunguzi wetu kwa umakini na usiri mkubwa kuhakikisha haki inatendeka,” alisema Msumile.
Uchaguzi mdogo wa madiwani utafanyika Jumapili ijayo katika kata 19 nchini.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa