Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kakusulo Sambo amewajia juu
polisi kwa tabia yao ya kutumia nguvu na kukiuka sheria wanapochukua
maelezo ya washtakiwa na kusababisha ushahidi muhimu kupotea.
Jaji Sambo alitoa kauli hiyo juzi wakati akitoa
uamuzi mdogo katika kesi ya mauaji ya polisi wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU), PC Michael Milanzi inayowakabili raia wawili wa Kenya na
Watanzania 10.
Uamuzi huo ulitokana na pingamizi la mawakili wa
utetezi baada ya upande wa mashtaka kuomba maelezo ya ungamo la
mshtakiwa wa pili, Peter Kimani yapokelewe mahakamani kama kielelezo.
Maelezo hayo yalichukuliwa Agosti 13, 2007 na
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Jumanne Shimbos baada ya mshtakiwa huyo
kuomba apelekwe kwa mlinzi wa amani ili aweze kukiri makosa yake.
Mawakili wa Utetezi, Majura Magafu, Profesa Jonas
Itemba, Faustine Matemu, Ralph Njau na Martin Kilasara walipinga maelezo
hayo wakisema yalichukuliwa nje ya muda ulioidhinishwa kisheria.
Kwa mujibu wa mawakili hao, kifungu cha 50 na 51
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinataka maelezo ya
mtuhumiwa yachukuliwe ndani ya masaa manne tangu kukamatwa.
Endapo polisi anayechukua maelezo hayo ataona
anahitaji kuendelea kumhoji mtuhumiwa, anapaswa kuomba kwa bosi wake na
ombi hilo liandikwe kwenye maelezo. Hata hivyo, mawakili hao walisema
maelezo ya ungamo ya mshtakiwa wa pili ambaye ni raia wa Kenya,
yalichukuliwa na mlinzi wa amani siku 13 baada ya kukamatwa kwake Julai
20, 2013.
Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya anayeendesha
kesi hiyo akisaidiwa na wakili Stella Majaliwa na Ignas Mwinuka,
walisema vifungu hivyo havizungumzii maelezo ya ungamo kwa mlinzi wa
amani.
Katika uamuzi wake mdogo, Jaji Sambo alikubaliana
na hoja ya mawakili hao wa Serikali, lakini akasema ipo kesi ya mifano
ya Mahakama ya Rufaa iliyojumuisha pia maelezo ya mlinzi wa amani.
Jaji Sambo aliwalaumu moja kwa moja polisi kuwa
wanatumia nguvu wakati wa kuchukua maelezo ya mtuhumiwa anayekiri kosa
badala ya kufuata maelezo ya vifungu hivyo vya CPA.
Kwa mujibu wa Jaji Sambo, dosari hizo zinazofanywa
na polisi zinawapa shida mawakili wa Serikali kutetea hoja mahakamani
na kufanya ushahidi muhimu kama huo kutochukuliwa na mahakama.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment