Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkazi mmoja wa Same mkoani Kilimanjaro anashikiliwa na polisi
kwa tuhuma za kuwabaka watoto wake wawili kwa kipindi cha miaka minne
mfululizo.
Mwanamume huyo anatuhumiwa kuwageuza watoto hao wake zake tangu alipoachana na mkewe mwaka 2010.
Bibi wa watoto hao, Joyce Mmbaga alisema taarifa
za ukatili huo alizipata kwa mmoja wa wajukuu zake hao ambaye kwa sasa
ana umri wa miaka 14. Alimkariri mjukuu huyo akisema kwamba amekuwa
akibakwa na baba yake mzazi tangu mwaka 2011 na kila anapomfanyia unyama
huo alimtishia kumuua kama angemwambia mtu.
Mmbaga alisema siri hiyo ilivuja baada ya kuanza
jitihada za kumtafutia shule mjukuu huyo ili arudie darasa la saba baada
kushindwa kufaulu. Alisema mtoto huyo alimweleza kwamba hakuwa tayari
kusoma shule za Same Mjini na kutaka kupelekwa mbali na mazingira ya
nyumbani.
Bibi huyo alieleza kuwa alitii ombi la mjukuu wake
na kumpeleka Kata ya Gonja ambako aliendelea na masomo lakini baba yake
alikuwa akimpigia simu kupitia kwa mama anayeishi na mtoto huyo akitaka
mtoto wake arudi nyumbani.
“Baba yao alidai mtoto arudi nyumbani na akaanza
kumtukana mama aliyekuwa akiishi na huyu mtoto hali iliyomfanya mama
huyo aanze mipango ya kumrudisha nyumbani kuepuka matusi ya baba yake.
Lakini mtoto alivyosikia anarudishwa kwa baba yake alilia sana na
kunyanyua Biblia juu akiomba Mungu amchukue ili aachane na maisha ya
kuishi na baba yake,” alisema.
Alisema kilio kile kilimfanya mama huyo kukaa na
mtoto huyo na kuanza kumhoji sababu ndipo alipodai kuwa baba yake
amekuwa akifanya naye mapenzi yeye na mdogo wake tangu mama yao
alipoondoka na kuwaacha.
Mmbaga alisema baada ya maelezo hayo walipiga simu
polisi ambao waliwachukua watoto hao na kuwahoji kisha kuwapeleka
Hospitali ya Same kwa uchunguzi.
Imeelezwa kwamba taarifa ya kidaktari ilionyesha kuwa watoto hao wamebakwa kwa muda mrefu kiasi cha kuharibu maumbile yao.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka
Moita alisema jeshi lake linaendelea na uchunguzi na baba huyo
atafikishwa mahakamani muda wowote uchunguzi utakapokamilika.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment