Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
BODI
ya Utalii Tanzania (TTB), imempa ubalozi wa heshima wa utalii nchini
Marekani, Macon Dunnagan aliyeutangaza Mlima Kilimanjaro kwa miaka 35.
Akizungumza wakati wa kumpokea mtalii huyo aliyeupanda mlima
Kilimanjaro kwa zaidi ya mara 35 katika geti la Marangu, Ofisa Uhusiano
wa TTB, Augustina Makoye, alisema wameshawishika kumpa ubalozi wa
heshima raia huyo ya Marekani, kutokana na juhudi zake za kuutangaza
mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.
“Dunnagan amekuwa akitembelea majimbo mbalimbali nchini Marekani, kwa
ajili ya kushawishi na kuhamasisha watu kuupanda mlima Kilimanjaro kwa
kujitolea bila malipo yoyote, hivyo TTB imeona ni vema kumpa heshima ya
kuwa balozi wetu huko,” alisema Makoye.
Pia, Makoye alisema TTB kwa muda mrefu imekuwa haina wawakilishi wake
katika majimbo nchini Marekani, hivyo kumpata Dunnagan ni mojawapo ya
jambo muhimu katika kukuza sekta ya utalii hapa nchini kwa mataifa
mbalimbali.
Kwa upande wake, Dunnagan aliishukuru serikali ya Tanzania kwa
kuutambua mchango wake katika kukuza utalii wa nje na kuongeza kwamba,
huo ni mwanzo tu ataendelea kutoa ushawishi kwa watu wa Marekani kuzuru
Mlima Kilimanjaro.
Itakumbukwa kwamba Macon aliongozana na watalii tisa kutoka katika
klabu za ‘rotary’ nchini Marekani wakiwa na madhumuni ya kuchangisha
fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Polio.
Dunnagan na wenzake, walifanikiwa kuchangisha sh milioni 480
takribani dola 300,000 za Marekani, ambazo zimetolewa kwa ajili ya
kuwafikia watoto wenye matatizo hayo.
Naye Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Erastus
Lufungulo, alisema watalii wengi kutoka Marekani wamekuwa wakizuru
kivutio hicho kutokana na hamasa ya Dunnagan na kwamba, sekta ya utalii
imeendelea kukua hapa nchini kutokana na wageni wengi kutembelea
vivutio.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment