Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani Chadema, Mabere Marando akikata utepe
kuzindua Bendi ya Wanawake na Operesheni Amsha Wanawake Tanzania katika
viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Dar es Salaam jana. Bendi hiyo
itatumika kuhamasisha katika mikutano ya Ukawa.
Chadema imefanya mikutano mikubwa ya kuamsha wapigakura katika
mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Dar es Salaam na Tanga huku mwenyekiti
wake, Freeman Mbowe akisema mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete waliotangaza
nia ya kugombea urais ‘wanaivua nguo’ Serikali waliyomo kwa kueleza
maovu ya ndani.
Alisema mawaziri hao hawana sauti moja, kila mmoja
anazungumza lake kuikosoa Serikali kwa kuahidi kufanya mambo mazuri
tofauti na yale yanayofanywa na Serikali ya sasa ya Kikwete.
Hadi sasa makada 38 wa CCM wamechukua fomu za
kuomba kuwania urais, miongoni mwao wakiwamo Makamu wa Rais, Dk Mohamed
Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri 10 na naibu mawaziri
wawili.
Katika kutangaza sifa zao baadhi yao wamekuwa
wakijigamba watatatua kero za ufisadi, migogoro ya ardhi, kudorora kwa
uchumi na kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mbowe alisema
Chadema haiwezi kuiga mfumo huo kwa sababu wana utaratibu wao wa
kutangaza nia na kuchukua fomu.
Alisema ratiba yao ya kuchukua fomu za urais ilishatolewa na itaanzia Julai 20 hadi Julai 25, mwaka huu.
“Mawaziri wa Kikwete hawana sera, wamesahau kuwa
nao ni sehemu ya serikali hiyo iyo wanayoikosoa. Chadema tuna utaratibu
wetu wa kutangaza nia na kuchukua fomu, nafasi ziko wazi,” alisema
Mbowe.
Alipoulizwa wamefikia wapi kuhusu mgombea
atakayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Mbowe alisema bado wanafanya
mashauriano, muda wowote wakimaliza mgombea wa Ukawa atatangazwa.
“Hii ni vita, hatuwezi kumweka wazi mgombea wetu
kwa sababu bado ni mapema. Ukawa bado tunafanya consultations
(mashauriano), tukimaliza Watanzania watamjua mgombea wa Ukawa,”
alifafanua kiongozi huyo.
Mbowe alipuuza madai kuwa Ukawa inavunjika,
akisema haiwezi kuvunjika kama watu wanavyodhani hasa baada ya
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuchukua
fomu ya kuwania urais ndani ya chama chake.
Alisisitiza kuwa Ukawa haijazuia chama chochote
kuchagua mgombea urais kama walivyofanya CUF bali chama chochote
kitasimamisha mgombea wake kisha wagombea wote kushindanishwa na kumpata
mmoja wa Ukawa.
“Jambo hili tuliliweka wazi tangu awali,
kusimamisha mgombea wa chama siyo hatua ya mwisho, ni sehemu ya mchakato
wa kumpata mgombea wa Ukawa,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe hakuweka wazi tarehe ya kutangazwa kwa mgombea wa Ukawa kwa madai kwamba mashauriano yanaendelea.
Ataka mashine za BVR zizuiwe
Akiwa mkoani Kilimanjaro, Mbowe amewataka wananchi
kuzuia mashine za BVR endapo hadi kufikia leo kutakuwa na watu wengi
ambao hawajaandikishwa kwenye Daftari la Wapigakura.
Mbowe alisema hayo juzi jioni katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Shirimatunda.
“Kujiandikisha kwenye BVR ni haki na wajibu wa
kila Mtanzania. Yapo maeneo mashine ni chache. Ikifika kesho (leo)
mfanye tathmini ya idadi ambao hawajaandikishwa,” alisema Mbowe na
kuongeza;
“Ikiwa kutakuwepo na watu wengi hawajaandikishwa
basi mhakikishe haiondoki mashine hata moja hadi watu wote waandikishwe
kwa sababu hizi mashine zimenunuliwa kwa kodi zenu na si fadhila”.
Hata hivyo, Mbowe aliwataka viongozi wa kata
zitakazokuwa na idadi kubwa ya watu ambao hawajaandikishwa, wawasilishe
malalamiko mapema kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Kabla ya kufikia hatua hiyo mhakikishe mmepeleka
malalamiko NEC. Aliyetenga siku saba za kujiandikisha ni mwanadamu na ni
huyo huyo anayeweza kuongeza siku,” alisisitiza Mbowe.
Amsha Wanawake Dar
Awali akizungumza katika uzinduzi wa mkakati wa
Amsha Wanawake kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu Dar es Salaam jana, Mjumbe wa
Kamati Kuu, Mabere Marando aliwataka makada wa vyama vya Ukawa kuacha
hofu juu ya hatima ya umoja huo kwa kuwa bado upo imara na
haujatetereka.
Alisema amekuwa akisikia kuwapo kwa “uoga uoga juu
ya msimamo wa Ukawa…kuna uvumi uvumi unaendelea baada ya juzi
mhemishiwa Profesa Lipumba kuchukua fomu... ule ni urataratibu wa
kawaida ambao viongozi wa juu wa Ukawa walikubaliana kuwa kila chama
kifuate taratibu za chama hicho hata Chadema tutafanya hivyo, NLD, CUF
na NCCR-Mageuzi,” alisema.
“Ukawa ipo imara…mimi nipo katika ngazi za juu za
maamuzi, hatujatetereka, tutawapa Watanzania mgombea mmoja wa kiti cha
urais, mmoja udiwani na ubunge…hakuna kitakachobadilika, Watanzania
msiwe na wasiwasi,” alisema Marando huku akishangiliwa.
Wabunge washambulia Manyara
Katika hatua nyingine, wabunge saba wa Chadema na
mmoja wa NCCR-Mageuzi jana waliushambulia Mkoa wa Manyara na kuendesha
mikutano ya hadhara kwa lengo la kuhamasiha wananchi wajiandikishe
kwenye BVR.
Wabunge hao ni Joseph Selasini (Rombo), Rose
Kamili, Pauline Gekul, Joyce Mukya, Cecilia Pareso , Grace Kiwelu (wote
viti maalumu) na Mbunge wa NCCR Kasulu Mjini, Mosses Machali.
Wabunge hao ambao awali walikuwa katika mikoa ya
Kilimanjaro na Arusha jana walitembelea kata za Maskta, Endasak,
Maeskroni na Mingenyi na mbali ya kuhamasisha wananchi wajiandikishe
waliwataka waiondoe CCM ifikapo Oktoba.
Akizungumza katika mikutano hiyo, Kiwelu aliwataka
wananchi wa eneo hilo kumchagua mbunge wa Chadema kwani ndiye
atakayeweza kuwaletea maendeleo.
“Nawapa pole wananchi wa Hanang’ kwani mlipata
viongozi wakubwa kama Frederick Sumaye aliyekuwa waziri mkuu kwa vipindi
viwili lakini hakuna hata barabara kwenye jimbo lenu kwani njia
wanayopitia ng’ombe ninyi ndiyo mnapita,” alisema Kiwelu na kuongeza.
“Tumepita kwenye barabara ambayo wanapita ng’ombe
na maji mnayotumia siyo safi wala salama, kwetu Kilimanjaro kuna huduma
bora ikiwamo ya umeme, hospitali na maji kutokana na wananchi kuichagua
Chadema.”
Kwa upande wake, Gekul alisema wananchi wa mkoa wa
Manyara, wamechoshwa na CCM hivyo wamejipanga kikamilifu kuhakikisha
wanaiangusha Oktoba.
“Hatutaiondoa CCM kwa rungu wala fimbo ila
tutaiondoa kwa kutumia kura za wananchi, nawaomba wananchi wote kama mna
hasira kutokana na huduma mbovu zinazotolewa na CCM ichagueni Chadema,”
alisema Gekul.
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini aliwataka wakazi
wa eneo hilo kutomchagua tena mbunge wa jimbo hilo, Mary Nagu kwa kuwa
ameshindwa kuwaletea maendeleo japokuwa amekuwa waziri kwa kipindi
kirefu.
“Mimi nimetokea Mkoa wa Kilimanjaro na kule kuna
maendeleo mengi na huduma za kijamii na barabara za lami yeye Nagu
amekuwa mbunge wenu kwa miaka kumi lakini ameshindwa kuwaleta hata
maji,” alisema Selasini.
Machali aliwataka wananchi wa jimbo hilo kuchagua
wagombea wa Ukawa ili wapate maendeleo kwa kuwa licha ya Hanang’ kuwa
eneo zuri lenye rutuba na mifugo mingi lakini wananchi wake wanaishi
kwenye lindi la umaskini.
“Hakuna sababu ya kuendelea kuichagua CCM kama wameshindwa
kuleta maendeleo, hivyo ninyi wenyewe ndiyo mnao maamuzi ya ama
kuendelea kunyonywa kwa miaka yote au kupata ukombozi kwa kuchagua
Ukawa,” alisema Machali.
Mwalimu na vyuo vikuu
Naibu katibu mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Salum
Mwalimu amewakumbusha vijana wa vyuo vikuu kusimamia kupatikana kile
alichokiita uhuru wa pili wa nchi wenye lengo la kuwakomboa Watanzania
kutoka maisha magumu.
Mwalimu aliyasema hayo jana mjini Lushoto wakati
akiongoza mahafali ya wanafunzi wanachama wa Chadema wa Chuo Kikuu cha
Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu) alikokabidhi vyeti kwa wahitimu.
Mwalimu alisema kuna ushawishi mkubwa unaofanywa
na CCM kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kwa kumwaga fedha na ahadi za vyeo na
ajira ili kuwapumbaza vijana kuondoka katika mstari wa harakati.
Alisema Serikali ya Ukawa itatatua changamoto zilizopo elimu ya juu
katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano.
Chanzo:Mwnanchi
Chanzo:Mwnanchi
0 comments:
Post a Comment