Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Freeman Mbowe akihutubia umati wa wananchi wa Jimbo la Hai katika mji mdogo wa Bomang’ombe jana.
Hai. Siku moja baada ya kuhukumiwa kulipa faini Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la shambulio la kawaida dhidi ya aliyekuwa mwangalizi wa ndani wa uchaguzi mkuu uliopita, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametangaza kuwania tena ubunge katika jimbo hilo.
Mbowe aliyeepuka kwenda jela kwa kulipa faini hiyo juzi, alitangaza uamuzi huo jana alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika eneo la stendi ya zamani mji mdogo wa Bomang’ombe, Kilimanjaro.
Mwenyekiti huyo alifikia hatua hiyo baada ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo kumshinikiza agombee ubunge na kumchangia Sh800,000 za kuchukua fomu ambayo ndani ya Chadema hugharimu Sh250,000.
“Nashukuru kwa walioanzisha wazo hili lakini zaidi ninawashukuru waliojitolea kunichangia fedha. Nimekubali nitagombea ubunge katika uchaguzi ujao,” alitangaza Mbowe na kufanya uwanja kulipuka kwa shangwe.
Mbowe aliyeambata na wabunge kadhaa akiwamo Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini, alijinasibu kuibuka na ushindi wa kishindo yeye na chama chake katika uchaguzi ujao kuanzia jimbo la Hai na katika majimbo yote ya Mkoa wa Kilimanjaro.
“Kama sheria ingekuwa inaruhusu ningefurahi iwapo CCM ingesimamisha wagombea zaidi ya 10 katika Jimbo la Hai ili wapambane na mimi kwa sababu mgombea mmoja pekee siyo saizi yangu,” alijinasibu Mbowe.
Hukumu dhidi yake
Akizungumzia hukumu iliyomtia hatiani na kuhukumiwa faini au kifungo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni alisema alikusudia kwenda jela kuwakilisha mamilioni ya Watanzania wanaosota huko “kwa kesi na hukumu za kipuuzi”.
“Kama kesi ya mtu mwenye dhamana ya uwakilishi wa wananchi kwa nafasi ya ubunge inaweza kuendeshwa kwa zaidi ya miaka minne na hukumu kutolewa katika mazingira tatanishi kama ilivyokuwa kwangu, Watanzania wa kawaida wanateseka kiasi gani?” alihoji Mbowe.
Alidai kuwa baada ya kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja au faini ya Sh1,000,000, Hakimu Denis Mpelembwa amepandishwa cheo kuwa hakimu mkazi na kuhamishiwa mkoani Kagera, siku moja tu baada ya hukumu.
“Kilichokuwa kinatafutwa ni namna ya kumzuia Mbowe asigombee ubunge Hai kwa sababu CCM wanajua nguvu yangu. Wamekosea sana kwa sababu hukumu ile hainizuii kugombea. Nitaombea na nitashinda kwa kishindo,” alisema.
“Ninao wanasheria mahiri ambao baada ya kupitia hukumu yangu kwa harakaharaka, wamenihakikishia kwamba adhabu ile hainizuii kugombea na wanaendelea na taratibu nyingine za kisheria kuiomba Mahakama Kuu kuitangaza kuwa batili,” alisema.
Atoa gari la taka
Katika tukio jingine, mbunge huyo alikabidhi gari na mtambo wa kukusanya na kusindika taka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wenye thamani ya zaidi ya Sh200 milioni.
“Gari hili nimelinunua kwa fedha zangu na kulipa gharama zote na ushuru baada ya Serikali kuniwekea mizengwe. Nalikabidhi kwa halmashauri kusaidia kuzoa taka ili kuweka jimbo letu katika hali ya usafi kama ilivyo kwa Manispaa ya Moshi,” alisema Mbowe.
Wabunge wanena
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wabunge waliohudhuria mkutano huo, Pauline Gekul, Grace Kiwelu, Rose Kamili na Joseph Selasini waliwaomba wakazi wa Hai kuhakikisha Mbowe anarejea tena bungeni kutokana na uwezo wake wa kiuongozi.
“Ili tufanikishe lengo la kumrejesha Mbowe bungeni na wagombea wengine wa Chadema, mnatakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na kujitokeza kupiga na kulinda kura Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Gekul.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment