Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwigizaji maarufu wa tamthilia ya Isidingo The Need, Jack
Devnarain maarufu kwa jina la uigizaji la Rajesh Kumar, amefanikiwa
kufika kilele cha Uhuru cha Mlima Kilimanjaro.
Rajesh,
ambaye ni raia wa Afrika Kusini, pamoja na wenzake 36 walipanda mlima
huo kuanzia Julai 14, kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Hayati Nelson
Mandela wa Afrika Kusini.
Mbali na kuadhimisha siku
hiyo muhimu kwa Taifa la Afrika Kusini, pia walipanda kwa ajili ya
kuchangisha fedha za kusaidia afya za watoto wa kike 272,000 wa nchi
hiyo na Tanzania.
Mratibu wa Taasisi ya Mandela ya
Trek4 Mandela nchini, Honest Minja alisema jana kwamba Kumar na wapanda
mlima wenzake 31 kati ya 37 walifanikiwa kufika kileleni.
Mhifadhi
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa), Erastus
Lufungulo alisema kati ya watu 37 waliopanda mlima, 32 walifika kileleni
na watano waliishia njiani.
“Wageni 32 wa Trek4
Mandela wamefika kileleni akiwamo msanii wa Isidingo. Watatu waliishia
kituo cha Kibo na wawili waliishia kati ya Kibo na kilelele cha
Gilmans,” alisema.
Kundi hilo la wapanda mlima
lilimjumuisha mpanda milima wa kimataifa Sibusiso Vilane ambaye ni
Mwafrika wa kwanza kupanda mlima Everest ambao ni mrefu kuliko yote
duniani.
Jana walitarajiwa kushuka hadi Kituo cha
Horombo kilichopo urefu wa mita 3,720 na leo walitarajiwa kushuka hadi
Mandara mita 2,700 na baadaye hadi lango kuu la Kinapa lililopo Marangu.
Chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment