Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro Saidi Meck Sadik ametoa rai kwa watumishi wa
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kubuni mbinu mpya za kuwahudumia
wanachama wao ili kuhamasisha watanzania wengi kujiunga na mfuko huo.
Rai
hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya wa Siha Dkt. Charles Mlingwa kwa niaba
ya Mkuu wa Mkoa alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa
mfuko huo uliofanyika Mkoani humo.
Mhe.
Meck Sadik amesema kuwa Baraza la wafanyakazi ndiyo chombo sahihi cha
uwakilishi wa sauti za watumishi katika kupanga malengo ya Taasisi pia
ni chombo cha kutatua migogoro ya kikazi na hivyo kumaliza mapema
tofauti zinazojitokeza katika sehemu za kazi kabla hazijaathiri
utendaji.
“Kutokana
na umuhimu wa huduma zenu kwa umma, Baraza la Wafanyakazi la Mfuko wenu
linatakiwa lichukue sura mpya na kuwa ni mahali pa ubunifu na kisima
cha kuibua mbinu mpya za kuwahudumia vizuri wanachama wenu na kujua
namna gani mtaendelea kuwavutia Watanzania wengi zaidi kujiunga na
Mfuko”,alisema Meck Sadik.
Mhe.
Meck Sadik ameongeza kuwa anawapongeza kwa ubunifu wao wa kubuni
mipango mbalimbali ya uchangiaji inayolenga kuwafikia watanzania wa
makundi mbalimbali kulingana na hali zao za vipato na uwezo wao wa
kuchangia.
“Hali
halisi ya uchumi wa watanzania mnaifahamu, siyo watu wengi wenye uwezo
wa kugharamia matibabu kwa fedha taslimu hivyo, huduma za matibabu
kupitia Mfuko huu ni ukombozi mkubwa kwa kundi kubwa la watanzania”,
alisema Meck Sadik.
Aidha, Mhe. Meck Sadik amewakumbusha wajumbe wa Baraza hilo
kuwa wao ni kiungo muhimu kati ya wafanyakazi na uongozi wa Mfuko kwa
hiyo, wana wajibu wa kuyaelewa malengo ya Taisisi yao kiutendaji na
kuyawasilisha kwa wafanyazi wenzao wakiwa kama wamiliki wa kile
walichokubaliana na uongozi kuwa ndiyo dira na mwelekeo wa taasisi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernald Konga amesema kuwa mfuko
huo utaendelea kushirikiana na Serikali, kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupunguza au kumaliza
kabisa tatizo la upungufu wa dawa nchini.
“Tunajua
kuwa upungufu wa dawa katika vituo vya matibabu umekuwa ni mojawapo ya
kero kubwa katika sekta ya afya. Ili kuondokana na kero hiyo, Mfuko
umeanza kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na upungufu huo kwa
kuanzisha mpango maalumu wa kutoa mikopo ya dawa kwa watoa huduma
waliosajiliwa ili kuhakikisha kuwa wanachama wetu na watanzania kwa
ujumla wanapata dawa kila wanapokwenda kupata huduma za
matibabu”,alisema Konga.
Chimbuko la Mabaraza ya Wafanyakazi linatokana na Agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970 lililoagiza kuwa mahali popote penye wafanyakazi wa kudumu kumi na kuendelea panatakiwa pawe na chombo cha kuwawakilisha.
0 comments:
Post a Comment