INAELEZWA kuwa tatizo la uhaba wa sukari kwa mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha, Manyara, Tanga na Singida, limekwisha baada ya Kiwanda cha
kuzalisha sukari cha TPC cha wilayani hapa kuzalisha tani 8,825 tangu
kilipoanza msimu mpya wa uzalishaji Juni 14, mwaka huu.
Hivi karibuni upungufu wa sukari nchini ulisababisha wananchi
kuitafuta bidhaa hiyo kwa bei ya juu, kutokana na baadhi ya viwanda
kusitisha uzalisha kwa muda wa miezi mitatu kwa lengo la kupisha
matengenezo, pamoja na mawakala kuhodhi bidhaa hiyo kwa lengo la kuiuza
kwa bei ya ulanguzi.
Taarifa ya kumalizika kwa tatizo la upatikanaji wa sukari, ilitolewa
jana na Ofisa Utawala wa Kiwanda cha Sukari TPC, Jaffari Ally, wakati
viongozi wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), walipotembelea kiwanda hicho kukagua utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2015/2020.
Ally alisema kati ya tani 8,825 ambazo zimezalishwa katika msimu huu
mpya, tayari jumla ya tani 7,800 zimeshaingizwa sokoni kwa ajili ya
matumizi ya wananchi, ambapo kwenye ghala wamebakiwa na tani zaidi ya
1,000.
Alieleza kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha sukari tani 450
kwa siku, ambapo kwa siku moja husambaza jumla ya tani 375, huku mikoa
ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara ikipata tani 270 na tani 105
zikisambazwa kwenye mikoa ya Tanga na Manyara.
Alisema , kwa msimu wa mwaka 2015/2016 kiwanda hicho kiliweza
kuzalisha jumla ya tani 96,000 za sukari, ambapo kwa msimu mpya wa mwaka
2016/2017 kiwanda hicho kinakusudia kuzalisha tani 105,000 za sukari,
ambapo alieleza kwa miaka mitano ijayo kiwanda hicho kitafikia
uzalishaji wa tani 120,000.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kilimanjaro, Deogratius
Rutta, alisema kiwanda cha TPC kina umuhimu mkubwa katika kutoa huduma
muhimu ya sukari, kama Ilani ya chama hicho inavyotoa kipaumbele kwenye
sekta ya viwanda.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment