Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Hospitali
ya Wilaya ya Siha iliyopo mkoani Kilimanjaro imetatua tatizo kubwa la
upatikanaji wa dawa lililokuwa linaikabili hospitali hiyo na kusababisha
wagonjwa kuhangaika kutafuta huduma hiyo katika maduka mbalimbali ya
watu binafsi, huku dawa hizo zikiuzwa kwa bei kubwa tofauti na ya
hospitali hapo.
Akizungumza hivi karibuni kwa
njia ya simu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Bw. Andew Method, alisema ni
kweli hospitali hiyo ilikua na uhaba mkubwa wa dawa hali iliyosababisha
usumbufu mkubwa kwa wagonjwa lakini zimefanyika jitihada kadhaa na kwa
sasa hospitali hiyo imetatua tatizo hilo kwa asilimia 70.
“Tayari
tulishaagiza dawa, na nyingi tulizokosa Bohari Kuu ya Dawa, tuliziagiza
kutoka kwa wazabuni na tunatarajia kuzipata kabla ya mwisho wa wiki hii
kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa wanaokuja kutibiwa katika hospitali
yetu na tunaamini zitasaidia kupunguza tatizo kwa asilimia 70 alisema
Bw. Method
Aliongeza
kuwa, waliagiza dawa za aina mbalimbali ikiwemo za “antibiotics” na za
kutuliza maumivu pamoja na vifaa tiba ambapo vyote kwa pamoja
vimegharimu fedha kiasi cha shilingi milioni 10.
Aidha, Bw. Method alisema kuwa hospitali hiyo imeandaa mikakati kadhaa ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu, ambapo tayari wanajindaa na taratibu za kufanya manunuzi ya dawa kutoka katika Bohari Kuu ya Dawa ikiwa ni pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya hiyo.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment