Na Jovina Bujulu-MAELEZO
Ni
miaka 17 tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki dunia. Ingawa
amefariki lakini fikra zake bado zinaishi kama alivyowahi kusema
mwanazuoni mmoja Seneta wa zamani wa Arkansas Bruce Holland “viongozi
mahiri hawafi wanaishi milele kupitia fikra zao na maisha yao”.
Kwa
kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere kupitia fikra zake mnamo mwaka 2012
watatafiti watatu walibuni wazo la kufanya utafiti kuhusu fikra na
falsafa za Mwalimu Nyerere, Wanazuoni hao ni Profesa Issa Shivji,
Profesa Saida Yahaya Othman na Dkt. Ng’anzi Kamata.
Wanazuoni
hao walihitimisha utafiti huo kwa kuandika bayografia ya Mwalimu
Nyerere ambapo walianzisha kavazi la Mwalimu Nyerere ambalo ni kituo
huru kilichoanzishwa mwaka 2014 ndani ya Tume ya Taifa ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH). Kavazi hilo lilizinduliwa mwaka 2015 na Rais
Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa.
Akizungumzia
utafiti wa Bayografia (Wasifu) ya Mwalimu Nyerere, Dkt Bashir Ally
ambaye ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Kavazi hilo alisema kuwa
ingawa watu mbali mbali wameandika bayografia ya Mwalimu Nyerere,
utafiti uliofanywa na wanazuoni hao watatu ni wa kwanza na wa kipekee
uliofanywa kwa kina tofauti na Bayografia za watu wengine.
Dkt.
Bashir anaendelea kusema kwamba wanazuoni hao wanaendelea kukusanya
taarifa mbali mbali za Mwalimu Nyerere, na nyaraka nyingi kutoka vyanzo
mbali mbali na kuzihifadhi katika Kavazi.
“Taarifa
za nyaraka zinazohusu kazi na maisha ya Mwalimu zinazopewa uhai kwa
kujadiliwa na kudadisiwa na watafiti wengine ndani na nje ya nchi hasa
vijana kwa sababu zinabeba historia ya nchi”. anaongeza Dkt. Bashir.
Kavazi
la Mwalimu Nyerere limetafsiriwa kama ni mahali maalumu ambapo
kumbukumbu za machapisho ya Mwalimu zimekusanywa na watafiti na
kuhifadhi pamoja. Kavazi hilo linatoa fursa kwa watafiti kubuni fikra mpya zenye misingi ya fikra za Mwalimu Nyerere.
Fikra
hizo zinatumika kama nyenzo muhimu katika kufanya utafiti za kisayansi
zitakazowezazesha nchi kupiga hatua za maendeleo kiuchumi kwa kuongeza
ubunifu katika rasilimali kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote.
Kavazi la Mwalimu ambalo linatumika kama kituo cha kuhifadhia na kuzipa uhai fikra zake limekwisha chapishwa machapisho matatu na mijadala mbalimbali.
Machapisho hayo ni ushairi ambao Mwalimu Nyerere aliouandika katika miaka ya 1950 na 1960, uanazuoni wa Mwalimu na insha tatu za kifalsafa na mjadala wa Pan-African Nationalist or Nationalist Pan-Africa.
Aidha,
Kavazi la Mwalimu limefanya Mhadhara tarehe 28, mwezi Septemba, 2016
ambapo mgeni rasmi alikuwa Mhe. Joseph Warioba ambaye ni Waziri Mkuu Mstaafu.
Mhadhara huo ulihusu elimu ya juu katika maendeleo ya Afrika na uliambatana na ufunguzi wa hifadhi ya Nyaraka ya Mwalimu Nyerere na uzinduzi wa chapisho la 4 la kavazi.
Akizungumzia
shughuli za Kavazi la Mwalimu Dkt. Bashir anasema kwamba ni pamoja na
kuhifadhi nyaraka zilizokusanywa na waandishi wa bayografia ya Mwalimu
Nyerere ili zitumiwe na watafiti, kutoa nafasi ya mjadala ya kizuoni na
kimkakati juu ya masuala muhimu ya maendeleo ya jamii, na kuandaa na
kuendesha mafunzo ya nadharia na mbinu za utafiti wa masuala ya
maendeleo ya jamii.
Aidha,
Dkt. Bashir anasema kwamba Kavazi la Mwalimu linatoa mafunzo kwa
wanazuoni na wasomi chipukizi waliopo kwenye taasisi za elimu ya juu na
asasi zisizo za kiserikali.
“Kavazi
limekwishafanya mafunzo kwa vijana ambayo yaliangalia rasilimali,
dhana, na nadharia mbalimbali na mbinu za kiutafiti ambazo zinawapa
maarifa na uwezo wa kuendeleza utafiti”. Anasema Dkt Bashir.
Wafadhili
wa Kavazi la Mwalimu ni pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) ambao walichangia fedha za awali, Taasisi ya Kijerumani ya Rossa
Luxemburg na watu mbalimbali.
Kavazi la Mwalimu limeanzisha mfuko maalumu (Endoworment Fund)
ambao utazalisha fedha za kujiendesha, hata hivyo wananchi wanaombwa
kuendelea kujitokeza kuchangia mfuko huo ili kukuza na kuendeleza kazi
za Kavazi.
Akizungumzia
mapokeo ya Kavazi la Mwalimu Dkt. Bashir anasema ni mazuri kwa sababu
viongozi mbalimbali wamekwisha tembelea Kavazi hilo wakiwemo Marais
Wastaafu Mhe. Benjamini Mkapa, Mhe. Ally Hassan Mwinyi na Mkurugenzi wa
Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku na ujumbe wake.
Viongozi wengine waliotembelea Kavazi hilo ni pamoja na Mawaziri Wakuu wastaafu
Mhe Cleopa David Msuya, Jaji Joseph Sinde Warioba, Dkt Salim Ahmed
Salim na wanasiasa mbalimbali wakiwemo waliofanya kazi na Mwalimu
Nyerere ambao ni Mze Geroge Kahama na Mzee Kingunge Ngombale Mwiru
familia ya Mwalimu Nyerere pamoja na wananchi mbalimbali.
Alisifu
ushirikiano wanaoupata kutoka Makumbusho ya Taifa, Taasisi ya Mwalimu
Nyerere na baadhi ya vyombo vya habari kuwa umewawezesha kufanya kazi
yao kwa ufanisi, hasa kukusanya nyaraka na taarifa za Mwalimu Nyerere.
Naye
Mkurugenzi wa Kavazi la Mwalimu, Profesa Issa Shivji ametoa wito kwa
viongozi na wanasiasa mbalimbali waliofanya kazi na Mwalimu Nyerere
kupeleka nyaraka zao katika Kavazi kwajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa
tafiti mbali mbali.
Dkt. Bashir anamalizia kwa kuwakaribisha wananchi kutembelea Kavazi ili kujisomea nyaraka na kazi za Mwalimu na kufahamu historia ya nchi yetu. Aidha anasema kuwa hakuna tozo yoyote kwa wananchi wanaokwenda kutembelea Kavazi hilo.
Ama
kweli Mwalimu Nyerere alikuwa Mwanafalsafa hodari na makini sana ambaye
mawazo au falsafa zake zitakumbukwa vizazi hadi vizazi hasa suala la
kutetea wanyonge, usawa wa binadamu na upendo kwa wote bila kujali
itikadi, dini wala kabila la mtu.
0 comments:
Post a Comment