Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mgeni
rasmi katika uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Robert George, ambaye ni
Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Moshi, akisikiliza maelezo ya namna jiko
hilo linavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia
wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini – CAMARTEC, Mhandisi
Noela Byabachwezi. Kushoto kwa Noela ni mshiriki kiongozi wa mradi wa
Green Voices Moshi, Farida Makame. Wengine pichani ni washiriki wa
kikundi hicho. Uzinduzi wa jiko hilo lililotengenezwa na CAMARTEC kwa
ufadhili wa Green Voices ulifanyika hivi karibuni mjini Moshi.
Jiko
la umeme-jua ambalo limetengenezwa na CAMARTEC kwa ufadhili wa mradi wa
Green Voices Tanzania kwa ajili ya kikundi cha akinamama wa TAWOCA
Moshi. Jiko hilo linafaa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja
na uharibifu wa mazingira.
Wanakikundi
wa TAWOCA Green Voices Moshi wakihakikisha jinsi joto la jua
linavyosaidia kupika kwa kutumia jiko la umeme-jua. Kushoto ni mgeni
rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa
Ushirika wa Manispaa ya Moshi.
Mgeni
rasmi katika uzinduzi wa jiko la umeme-jua, Ofisa Ushirika wa Manispaa
ya Moshi, Robert George, pamoja na akinamama wakisikiliza maelezo ya
namna jiko hilo linavyofanya kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Uhawilishaji
Teknolojia wa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini –
CAMARTEC, Mhandisi Noela Byabachwezi.
Mhandisi Noela Byabachwezi, mwenye kofia kulia, akionyesha kwa vitendo jinsi jiko la umeme-jua linavyofanya kazi.
Ofisa
Ushirika wa Manispaa ya Moshi, Robert George – kulia – akisikiliza
maelezo mbalimbali ya akinamama wa TAWOCA Green Voices Moshi kabla ya
kuzindua jiko la umeme-jua.
Picha ya pamoja.
VIUNGA
vya ukumbi wa Aroma mjini Moshi vimesheheni akinamama wengi katika siku
hii ya Jumamosi, kama ilivyo kawaida kwa siku kama hiyo, ambapo wote
wanaonekana kuwa na nyuso za furaha kutokana na mijadala inayoendelea.
Lakini
tofauti na Jumamosi nyingine ambapo akinamama wa kikundi cha Wamama wa
Kahawa ambao ni wanachama wa Tanzania Women Coffee Association - TAWOCA
mjini humo kujadili masuala mbalimbali ya ujasiriamali, siku hii
inaonekana kuwa ya tofauti kwa sababu licha ya idadi ya akinamama
kuongezeka, lakini kuna tukio kubwa na muhimu ambalo limewakutanisha.
"Leo
tunazindua rasmi jiko la umeme-jua, yaani parabolic solar cooker,
ambalo kupitia udhamini wa mradi wa akinamama wa Green Voices, hatimaye
limeweza kupatikana baada ya jithada za miezi kadhaa," ndivyo anavyoanza
kuelezea Farida Makame, mshiriki kiongozi wa mradi wa Green Voices wa
kikundi hicho, huku akionyesha kifaa kinachofanana na dish kama la
satellite ambacho katikati yake kumewekwa sufuria inayong’aa kama taa
kubwa ya umeme.
Anasema
kwamba, jiko hilo linaweza kupika kila aina ya chakula kwa kutumia
mionzi ya jua ya moja kwa moja bila kuathiri mazingira.
"Kwa
kutumia jiko hili maana yake huhitaji kutafuta mkaa wala kuni, hivyo
kuokoa misitu ambayo inateketea kila siku kutokana na ukataji wa miti
kwa ajili ya kutafuta nishati ya kupikia," anaongeza.
Farida,
ambaye pamoja na akinamama wengine 14 – wakiwemo wanahabari watano
wanawake – walipatiwa mafunzo ya takriban miezi miwili jijini Madrid,
Hispania mapema mwaka huu wa 2016, anasema kwamba lengo la kubuni na
kutengeneza jiko hilo la umeme-jua ni kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi pamoja na kupambana na uharibifu wa mazingira.
Anaeleza
kwamba, haikuwa kazi rahisi kwake kukamilisha ubunifu wake, wazo ambalo
aliliwasilisha akiwa mafunzoni, na kwamba ndiyo maana mradi wake
umechelewa kutokana na kuhitaji teknolojia zaidi.
"Tumeanzisha
huu mradi baada ya kukaa na akinamama wa TAWOCA na kuwauliza changamoto
mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao, moja ya changamoto ni
upatikanaji wa kuni na mkaa, gesi na umeme.
"Kwahiyo
tukaangalia kama kuna njia mbadala ambayo akinamama wanaweza kuitumia
na ikawa nafuu na pia kiafya, kwa sababu njia ya kutumia umeme-jua ina
manufaa sana kiafya, kwa hiyo tukaungana na wenzetu wa Kituo cha Zana za
Kilimo na Teknolojia Vijijini, CAMARTEC, kwa sababu ndio watafiti wa
mashine na zana za kilimo, ili kutengeneza jiko hili linalotumia nishati
ya jua," anasema.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Uhawilishaji Teknolojia wa CAMARTEC,
Mhandisi Noela Byabachwezi anasema imekuwa ni fursa kubwa kwao kufanya
kazi na mradi wa Green Voices, kwani wameweza kutengeneza kwa mara ya
kwanza jiko hilo ambalo limewapa hamasa wahandisi wa kituo hicho
kuliboresha zaidi kwani linaonekana kuwa na manufaa makubwa.
Anakiri
kwamba, ingawa wanabuni teknolojia mbalimbali ikiwemo kutengeneza
majiko na makaushio yanayotumia umeme-jua, lakini hiyo ndiyo mara ya
kwanza kwa kituo hicho kutengeneza jiko linalotumia nguvu ya jua moja
kwa moja.
"Hivi
sasa tunafanya utafiti kama tunaweza kulitengeneza dogo lakini lenye
nguvu au kutengeneza jiko linaloweza kukunjwa na kuhifadhiwa kirahisi
kwa sababu hili ni kubwa na inakuwa shida ikiwa mtu hana nafasi kubwa ya
kuhifadhia," anasema Mhandisi Noela.
Akizungumzia
kuhusu ufanisi wake, Noela anasema kwamba, jiko hilo ni rafiki mkubwa
wa mazingira na lina uwezo mkubwa wa kupika na hata kuoka vyakula vya
aina zote ikiwa tu kutakuwepo na jua la kutosha.
Kwa
maeneo kame na yenye jua kali kama mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora,
Shinyanga na hata Dar es Salaam, jiko hilo linafaa sana kutumiwa bila
shida, anaongeza mhandisi huyo.
Aidha,
anafafanua kwamba, jiko hilo linaweza kupika chakula kwa ajili ya watu
wengi na kwamba ni jukumu la jamii kugeukia matumizi ya jiko hilo
lisilotumia mafuta wala nishati nyingine kwa sababu siyo tu linapunguza
gharama, lakini pia linaokoa misitu kwa vile miti haitakatwa ikiwa
watakuwa wanalitumia.
"Jambo
jingine la muhimu ni kwamba, upikaji kwa kutumia jiko la umeme-jua mara
nyingi hufanyika nje na katika mazingira ambayo yanahitaji matumizi
madogo ya mafuta na kuni, au hatari ya ajali za moto na inaokoa afya za
wanajamii, hususan akinamama pamoja na kuyalinda mazingira yetu,"
anaongeza Mhandisi Noela.
"Kama
unavyoliona, jiko hili limetengenezwa kwa vifaa maalum vikiwemo vioo,
ambavyo vinang’aa na kuakisi mwanga wa jua, vimepangwa kitaalam na
mwanga huu unapoakisiwa unakwenda moja kwa moja kwenye sufuria ambayo
kutokana na joto lake, chakula chochote kinachopikwa kinaiva bila
wasiwasi wowote. Kama jua litakuwepo la kutosha, joto linalozalishwa na
jiko hili linaweza kufikia hadi nyuzijoto 400 °C."
Kwa
mujibu wa mhandisi huyo, vyakula vinavyopikwa kwa kutumia jiko la aina
hiyo ni vyema vikawa katika maumbile madogo ili kusaidia kuiva haraka na
kwamba muda wa chakula kuiva unategemea na vifaa unavyotumia, kiwango
cha jua, na kiasi cha chakula kinachopikwa.
Faida
kubwa za utumiaji wa jiko la umeme-jua zinatajwa kwamba, mbali ya
kuokoa mazingira, ni uwezo wa kupika vyakula vigumu, kukaanga nyama,
kupika supu, kuoka mikate na kuchemsha maji kwa muda mfupi.
Hata hivyo, jiko hilo linahitaji zaidi uwepo wa jua, kwani ndiyo chanzo cha joto linalofaa kupikia.
Mmoja
wa wanakikundi hicho, Esther Moshi, amesema kupatikana kwa jiko hilo
kutawakomboa wanawake wengi ambao mara nyingi ndio wanaokabiliwa na
changamoto ya utafutaji wa nishati za kupikia kama kuni na mkaa.
"Tunashukuru
mradi wa Green Voices kwa sababu unalenga kumkomboa mwanamke kutokana
na adha ya upatikanaji wa nishati ya kupikia, kama majiko haya
yatatengenezwa kwa wingi na kila familia kulipata, hakika yatakuwa
mkombozi na yatasaidia kuokoa mazingira, " anasema.
Fatima
Aziz Faraji ni mwenyekiti wa Chama cha TAWOCA, amesema ni muhimu kwa
wanawake kuzidisha umoja wa vikundi ili waweze kusonga mbele na
akaupongeza mradi huo kwamba utakuwa mkombozi si kwa wanawake pekee,
bali jamii nzima.
Mgeni
rasmi katika uzinduzi wa jiko hilo, Robert George, ambaye ni Ofisa
Ushirika wa Manispaa ya Moshi, ameupongeza mradi wa Green Voices pamoja
na akinamama hao na akahimiza kuwa, ni vyema kutumia teknolojia ambazo
ni rafiki wa mazingira.
Amesema
akinamama ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya nishati za kupikia, na
kwamba ndio wanaoongoza kupata madhara kiafya, hasa wanapotumia mkaa na
kuni.
"Jitihada
hizi za wenzetu wa Green Voices zinapaswa kuongezwa, kwa sababu
zinalengo siyo tu kumkomboa mwanamke, bali kulinda mazingira yetu ambayo
yanazidi kuteketea kila uchao kutokana na ukataji wa misitu kwa
madhumuni ya kutafuta kuni na mkaa.
"Akinamama
wanaathirika sana, wengine utakuta macho mekundu kutokana na moshi wa
kuni, na wanapokuwa wazee ndio wanaoshambuliwa na watu wengine wasio na
utu kwamba eti ni wachawi kwa sababu macho yao ni mekundu, lazima
kutumia teknolojia mbadala kuwanusuru mama zetu, " alisema.
Hata hivyo, aliwataka akinamama hao kushikamana pamoja katika shughuli zao ili waweze kujiletea maendeleo, kwani umoja ni nguvu.
Kwa
upande wake, Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela
Balisidya, amesema, mradi wa jiko la umeme-jua ni sehemu ya miradi 10
inayotekelezwa chini ya Green Voices ambapo Tanzania ndiyo pekee
iliyopendekezwa kutekeleza mradi huo unaofadhiliwa na Taasisi ya Mfuko
wa Wanawake wa Afrika, , ambayo inaongozwa na makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega Sanz.
Hata
hivyo, taasisi hiyo inafadhili miradi 15 ya wanawake katika nchi 12
barani Afrika ambayo imeonyesha mafanikio, huku mradi wa Green Voices
ukitajwa kuwa na mafanikio makubwa katika kipindi kifupi.
Kwa
mujibu wa Bi. Secelela, Mradi wa Green Voices unatekelezwa katika mikoa
sita ya Tanzania Bara ambayo ni Dar es Salaam, Pwani, Mwanza, Kigoma,
Morogoro na Kilimanjaro.
“Miradi
hiyo ni kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi
lishe visiwani Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na
Pwani, ukaushaji wa mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani
Morogoro, usindikaji wa vyakula mbalimbali kutokana na muhogo mkoani
Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, na kilimo cha uyoga mkoani Dar es
Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi huu wa utafiti wa
jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanjaro,” anafafanua
Secelela.
Anasema,
lengo kubwa la mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama
kueneza ujuzi wao wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii
nzima ya kitanzania iweze kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika
kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Serikali
kupitia taasisi na idara zake zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na
Biashara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii imekuwa ikiendesha
program mbalimbali za mafunzo ya ufundi ikiwemo utengenezaji wa majiko
banifu na sanifu kama inayoendelea katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Malampaka wilayani Maswa.
Hata hivyo, bajeti ndogo imekuwa changamoto kubwa kukwamisha kuwafikia wananchi wengi na kuwapatia elimu ya aina hiyo.
0 comments:
Post a Comment