Imeandikwa na Flora Mwakasala, Moshi
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kilimanjaro kimeendelea kufanya
shangwe katika marudio ya uchaguzi mdogo baada ya kuibuka kidedea katika
uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji na vitongoji.
Katika marudio ya uchaguzi mdogo uliofanyika wiki iliyopita kwenye
vijiji vinne, vitongoji 19 na Wajumbe wa Serikali za Vijiji 53, katika
Jimbo la Mwanga CCM ilishinda nafasi zote, na juzi iliibuka kidedea kwa
kuchukua viti viwili vya Uenyekiti wa Vijiji.
Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Jimbo la Moshi Vijijini ambaye pia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Butamo Ndalahwa
alisema vijiji vilivyokuwa vikirudia uchaguzi ni vitatu, vitongoji 12,
pamoja na nafasi 14 za Wajumbe wa serikali ya kijiji cha Okaoni.
Ndalahwa alisema katika nafasi ya Wenyeviti wa vijiji CCM ilishinda
vijiji viwili ambavyo ni Mande na Mkomilo huku kijiji cha Msae Nganyeni,
kikichukuliwa na NCCR-Mageuzi, pia CCM imeshinda vitongoji tisa,
Chadema viwili na NCCR-Mageuzi wakiambulia kimoja, wajumbe wa kata CCM
ilishinda wajumbe 13, Chadema mjumbe mmoja.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema ushindi
unaopatikana katika marudio ya uchaguzi mdogo, unaonesha kuwa wakazi wa
Mkoa wa Kilimanjaro wamerudisha imani yao kwa CCM.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment