Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Kila
ifikapo Septemba 27 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya utalii
duniani. Maadhimisho hayo hufanywa na kila nchi ambapo kunakuwepo na
shughuli kadhaa zikiongozwa na malengo na kauli mbiu tofauti
zilizoazimiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UNWTO).
Mnamo
mwaka 2015, Mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa uliutangaza
mwaka 2017 kama Mwaka wa Kimataifa wa Utalii Endelevu kwa Maendeleo. Na
hivyo kuifanya kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni ‘Utalii Endelevu kwa
Maendeleo.’
Maeneo
matano ambayo yanaangaziwa na kufanyiwa kazi mwaka huu ni; Ukuaji wa
uchumi endelevu na wa pamoja; Ujumuishwaji wa jamii, ajira na kupunguza
umasikini; Ufanisi wa rasilimali, utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya
hali ya hewa; Amali za kiutamaduni, utofauti na urithi; na Maelewano ya
pamoja, amani na usalama.
Katika
kuunga mkono maadhimisho haya, Jumia Travel ikiwa ni mdau wa masuala ya
utalii Tanzania na Afrika kwa ujumla imekuwa ikifanya jitihada za
kukuza ufahamu juu ya maeneo na vivutio mbalimbali vya utalii nchini.
Hivi
sasa kuna kampeni inayoendelea kwa jina la ‘Destinations Campaign’
ikiwa inalenga kukuza ufahamu juu ya maeneo tofauti nchini ambayo
watanzania hawafahamu kama ni vivutio vya kitalii.
Tanzania
imebarikiwa kuwa na maeneo mengi lakini hayapewi kipaumbele wala
kutangazwa vilivyo. Na endapo ikiwa yanatangazwa, sio yote yanayopata
fursa sawa kama vile Zanzibar, Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti ambayo watu wengi nchini na duniani wanayafahamu.
Jumia
Travel imeamua kuitumia fursa ya kufanya kazi na maelfu ya hoteli
nchini na Afrika kuyaangazia maeneo hayo na sehemu ambazo wageni
wanaweza kulala. Kikubwa kinachofanyika ni kuwafahamisha watanzania juu
ya shughuli tofauti wanazoweza kuzifanya pindi wakitembelea maeneo hayo.
Mbali na hapo wamiliki na mameneja wa hoteli huhojiwa juu ya masuala
wanayoona yanaweza kuwavutia wateja kwenye hoteli zao.
Jitihada
za kukuza ufahamu na kutangaza maeneo mbalimbali nchini zinafanywa pia
na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). Bodi ya Utalii imekuja na mkakati na
mbinu mpya kwa kuyatenga maeneo ya usimamizi wa wanyama tofauti na ya
kawaida yaliyozoeleka na watalii wengi.
Kwa
mfano, hivi sasa TTB inafanya jitihada kubwa za kukuza maeneo matano
yaliyomo kwenye mpango wa usimamizi huo ambayo ni Burunge ipo Wilaya ya
Babati Mkoa wa Manyara, Randilen ipo Wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha,
Ikona ipo katika Wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara jirani na Hifadhi ya
Taifa ya Serengeti, Ipole ipo katika Wilaya ya Sikonge mkoa wa Tabora na
Mbomipa ambayo ni muunganiko wa vijiji zaidi ya 21 vya tarafa za Idodi
na Pawaga vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Kwa
kufanya hivyo inatoa fursa kwa watalii kuwa na machaguo ya sehemu za
kutembelea tofauti na yaliyozoeleka. Kwa sababu hata kwenye maeneo haya
watalii wanaweza kukidhi haja zao kwa kuwaona wanyama na kufanya
shughuli nyinginezo za kitalii.
Kwa
mujibu wa ripoti ya utalii ya mwaka 2016 iliyotolewa na Shirika la
Umoja wa Kimataifa la Utalii Duniani, Mwaka 2016 umethibitisha kuwa ni
mwaka mwingine wa mafanikio katika sekta ya utalii kimataifa licha ya
changamoto kadhaa. Idadi ya watalii kimataifa imekuwa kwa mwaka wa saba
mfululizo na kufikia bilioni 1.2, idadi ya ukuaji ambayo haijawahi
kutokea tangu miaka ya ‘60’ (1960). Ukuaji mkubwa zaidi umeonekana
kwenye sehemu za Afrika, Asia na Pasifiki.
Tunakukaribisha katika kuungana nasi na kusherehekea Mwaka wa Kimataifa wa Utalii Endelevu kwa Maendeleo 2017.
0 comments:
Post a Comment