Nora Damian
MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), imesema kuwa mchele uliokamatwa mkoani Kilimanjaro ni salama na unaweza kutumiwa na binadamu. Mchele huo uliokamatwa mwezi uliopita unadaiwa uliingizwa nchini kutoka nchi jirani na kusadikika kuwa hauna ubora na usalama unaokubalika.
Hatua hiyo inawasafisha watu waliohusika na kusafirisha mchele huo pamoja na kuusambaza, ikiwaacha huru.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza alisema matokeo ya uchunguzi wa kimaabara yameonyesha kuwa mchele huo unafaa kwa matumizi ya binadamu.
Alisema katika ukaguzi huo, jumla ya mifuko 150 yenye ujazo wa kilo 25 ilizuiliwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kilimanjaro na kwamba sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
“Ufuatiliaji wa mchele huo ulibaini kuwa mchele uliingizwa nchini kutoka nchi jirani pasipo kibali cha TFDA,”alisema Simwanza na kuongeza kuwa: “Hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya walioingiza mchele huo kinyume cha utaratibu.”
Ofisa huyo alisema kuwa ufuatiliaji wa mchele huo ulifanywa na kikosi kazi kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa, ambacho kilihusisha ofisa wa TFDA Kanda ya Kaskazini, maofisa afya kutoka Manispaa ya Moshi, maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Maofisa biashara na polisi.
Simwanza alisema kuwa katika udhibiti wa vyakula kutoka nje ya nchi, michakato mbalimbali hufanywa na TFDA ili kuwa na uhakika juu ya usalama wa bidhaa kwa kufanya tathmini na uchunguzi wa kimaabara wa sampuli za bidhaa husika.
Alifafanua kuwa baada ya kuzisajili na kujiridhisha juu ya usalama wake hutoa vibali vya kuingiza nchini, kufanya ukaguzi katika vituo vya forodha kabla ya kuingizwa nchini na maeneo ya kuuzia baada ya kuruhusiwa kuingizwa nchini.
Alitoa wito kwa wafanyabiashara kuzingatia taratibu za uingizaji wa chakula nchini ili kuepusha uwezekano wa kuingiza bidhaa ambazo zinaweza kuleta madhara ya afya kwa walaji.
Simwanza aliwataka wananchi na jamii pia kutoa taarifa pale wanapouziwa au kuhisi kuwepo kwa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba duni au bandia visivyokidhi viwango vya ubora na usalama.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment