Daniel Mjema, Rombo
VIGOGO watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, jana walitinga kizimbani mjini hapa kujibu mashitaka ya uhujumu uchumi.Watuhumiwa hao waliokuwa wakishikilia nyadhifa mbalimbali katika halmashauri hiyo, wanatuhumiwa kuisababishia Halmashauri ya wilaya hiyo hasara ya Sh29,910,000.
Washitakiwa hao na nyadhifa zao zikiwa kwenye mabano ni Joseph Ngoseki (Ofisa Elimu), Emmanuel Masele (Mweka Hazina wilaya) na Elias Mshana (Kaimu Mkurugenzi).
Wengine ni Erick Barongo ambaye ni mhasibu na Rahel Mshangila ambaye ni Ofisa Ugavi msaidizi wa Halmashauri hiyo.
Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mariam Lusewa aliamuru washitakiwa hao kwenda mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ikiwamo kutoa fedha taslim.
Masharti hayo ya dhamana yaliwataka washtakiwa kukabidhi mahakamani fedha taslimu Sh3 milioni kila mmoja au mali isiyohamishika iliyofanyiwa uthamini (valuation) na pia kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini dhamana ya maneno ya Sh3 milioni.
Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghella Ndimbo alidai kuwa makosa hayo yalitendeka kati ya Septemba na Oktoba 2007.
Katika kipindi hicho, washitakiwa wanadaiwa kutumia vibaya nafasi kwa kulipa malipo ya vifaa hewa vya kufundishia na kuipa faida isiyostahili kampuni ya Magoma Agencies.
Aidha katika shitaka linguine lililotendeka, watuhumiwa hao wanatuhumiwa kuisababishia halmashauri hasara ya Sh29.9 milioni.
Wakati mashtaka hayo yakisomwa mahakamani, mstakiwa wa kwanza, Ngoseki hakuwepo mahakamani kwa kuwa anashikiliwa mahabusu Gereza la Karanga.
Mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi katika mahakama ya Hakimu mkazi mjini Moshi ambako pia alishindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Lusewa aliamuru kuandikwa kwa hati ya kumtoa gerezani mtuhumiwa huyo ili aweze kusomewa mashitaka hayo na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Juni 27, mwaka huu.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment