Home » » Vigogo watano TRA wapandishwa kizimbani

Vigogo watano TRA wapandishwa kizimbani


Na Omary Mlekwa, Moshi
WATUMISHI watano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika wa kituo cha Holili, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, pamoja na wafanyabiashara wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kilimanjaro, wakikabiliwa na mashitaka 26 ya kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh bilioni 1.5
Washtakiwa hao ni Ally Mgumia, Giliard Ngowi ambao ni wahasibu wasaidizi katika kituo hicho, Pelagi Silayo, Mhasibu Mkuu wa Kituo hicho, Hamisi Kiula na Shukuru Jongo.

Wengine waliofikishwa mahakamani ni pamoja na wafanyabiashara Hemedi Saidi na Domisian Rwezura.

Akisoma hati ya mashitaka mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Saimoni Kobelo, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani hapa, Magella Ndimbo, alidai washtakiwa wote wanadaiwa kutenda makosa ya kumdanganya mwajiri wao kwa kutumia nyaraka mbalimbali ili kujipatia fedha.

Alisema makosa hayo, yamegawanyika katika maeneo matatu, ambayo ni kula njama za kumdanganya mwajiri wao kwa manufaa yao binafsi, kughushi nyaraka na kuhujumu uchumi.

Alidai mtuhumiwa wa tatu katika shitaka hilo, anakabiliwa na mashitaka 13 ya matumizi ya nyaraka mbalimbali na kumdanganya mwajiri wake kwa kuidhinisha malipo ya ushuru wa bidhaa zilizosajiliwa, bila kufuata taratibu kinyume na sheria namba 22 kifungu 11 ya mwaka 2007 ya TAKUKURU.

Alisema mshitakiwa wa kwanza katika shitaka hilo, Ally Mgumia anakabiliwa na mashitaka matatu, likiwamo la kughushi hati za malipo na kumdanganya mwajiri wake kwa kuhalalisha malipo ya bidhaa mbalimbali zilizosajiliwa na kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 32.

Alidai mshitakiwa wa pili, Gerald Ngowi, anakabiliwa na mashitaka matatu ya matumizi mabaya ya madaraka na kukiuka sheria halali kwa kumdanganya mwajiri wake, kwa kutumia mtandao ujulikanao kama SUDA na kuisababishia hasara mamlaka hiyo Sh milioni 13. 

Alisema, watumishi wengine, Hamisi Kiula na Shukuru Jongo, wanakabiliwa na tuhuma za kuruhusu mizigo iliyokuwa imesajiliwa kutoka bila kufuata taratibu, jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya Afrika Mashariki namba 1 ya mwaka 2005.

Alisema watumishi hao, walifanya makosa hayo kati ya Juni, 2007 na Septemba, 2009, wakiwa waajiriwa wa mamlaka hiyo.

Hata hivyo, washitakiwa wote walipelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambapo kila mmoja alitakiwa kuweka benki Sh milioni 93 au mali isiyohamishika. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 11, mwaka huu.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa