na Grace Macha, Moshi
ONGEZEKO la bei ya meno ya tembo na pembe za ndovu kwenye nchi za Bara la Asia, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matukio ya ujangili hapa nchini, imeelezwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), Allan Kijazi, alitoa kauli hiyo wakati akifungua semina ya waandishi wa habari Kanda ya Kaskazini juu ya uhamasishaji wa utalii wa ndani kwenye Hoteli ya kitalii ya Sal Sanero, Moshi.
Alisema meno ya tembo hununuliwa kwa wastani wa dola 1,000 kwa kilogram moja ( sawa na zaidi ya sh mil. 1,500,000) kwenye nchi za China, Japan, Taiwan na India ambazo uchumi wake umekua sana, jambo alilosema kuwa limechangia kuongeza mtandao wa ujangili .
Kijazi alisema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni kudhibiti ujangili huo ambao hufanyika kwa mtandao wa kimataifa unaowashirikisha majangili toka ndani na nje ya nchi huku wafadhili wao wakiwa kwenye nchi hizo za Bara la Asia.
Hata hivyo alisema (Tanapa) wamejizatiti kukabiliana na ujangili huo huku akisistiza umuhimu wa wananchi wote kushiriki kikamilifu kulinda rasilimali za Taifa kwa kutoa taarifa za majangili pindi wanapowabaini kwenye maeneo yao.
“Kwa sasa tunashirikiana na polisi wa kimataifa (Interpol) kufuatilia mtandao huu huko nje ya nchi ili tuweze kuwapata watuhumiwa sugu pamoja na vithibitisho vitakavyotuwezesha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema mkurugenzi mkuu huyo wa Tanapa wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Alisema wameamua kushirikiana na vyombo vya kiintelijensia vya kimataifa ili kuwawezesha kuwapata wale wanaofadhili mitandao hiyo ya kijangili, kwani tofauti na hivyo wataishia kukamata wapagazi waliotumwa kubeba nyara hizo, jambo ambalo haliwezi kumaliza tatizo hilo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment