Eliya Mbonea na Upendo Mosha, Kilimanjaro
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limesema linakabiliwa na changamoto ya mtandao hatari wa ujangili kutoka ndani na nje ya nchi.
Ujangili huo ulitajwa kuchangiwa zaidi na kukua kwa soko la pembe za faru na tembo katika nchi za China, India, Taiwani na Japan, ambapo kwa sasa bei ya kilo moja inakisiwa kufikia Dola 1,000 za Marekani kwa kilo moja kutoka Dola 50 za Marekani kwa kilo.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi, wakati wa semina ya waadishi wa habari wanaotoka Kanda ya Kaskazini katika mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
“Ujangili katika hifadhi zetu umeendelea kushamiri kutokana na mtandao mkubwa wa kimataifa wa ujangili unaoshamiri siku hadi siku.
“Naomba waandishi wa habari mtusaidie katika kufichua mitandao hii ili tuendelee kunusuru hifadhi zetu na dhidi ya majangili, hivi sasa soko limeonekana kuimarika zaidi katika nchi za Asia,” alisema Kijazi.
Alisema mtandao huo mkubwa wa ujangili wa kimataifa umekuwa ukifanya kazi kwa kushirikiana na baadhi ya wazawa nchini kufanya vitendo vya ujangili ikiwa ni pamoja na kuuwa wanyama akiwamo tembo na faru kwa lengo la kuchukua pembe za wanyama hao.
Alisema kutokana na kukabiliwa na changamoto hiyo, sasa TANAPA imejipanga kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuimarisha vitengo kadhaa vya ulinzi ndani ya hifadhi.
Katika hatua nyingine, aliwaomba waandishi wa habari kujikita katika kuandika habari sahihi za utalii nchini kwa ajili ya kujenga mtazamo mpya wa dhana ya utalii nchini.
Kwa upande wao, baadhi ya waandishi wa habari waliochangia mada iliyotolewa na Kijazi, Mwandishi Adamu Ihucha kwa upande wake aliweka wazi msimamo wake kuwa kupata habari za TANAPA ni kazi kubwa inayohitaji mlolongo mkubwa.
“Huu uzalendo mnaotaka tuwe nao waandishi wa habari ninashauri pia ungeanzia na kwa watendaji wenu kwa kuwa kupata habari za TANAPA ni sawa na kutafuta habari za magereza,” alisema Ihucha.
Alisema lengo la waandishi wa habari kuandika habari ambazo huonekana zina mrengo tofauti na shirika hilo huwa si kwa ajili ya kubomoa, bali hulenga kuwafahamisha wananchi juu ya rasilimali zao walizopewa na Mungu zinalindwa vipi na zinateketea vipi.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment