Daniel Mjema, Moshi
MAITI za wanawake watatu zimefukuliwa ili ziweze kupimwa vinasaba (DNA), kubaini kama mojawapo ni ya mwanamke anayedaiwa kuuawa kinyama na kuporwa mtoto wake.
Tayari, Muuguzi wa Hospitali ya Mawenzi, Candida Mafoy (49) na Katibu Muhtasi Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Beatrice Massawe (35) wameshtakiwa kortini wakituhumiwa kwa wizi wa mtoto huyo.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ameshindwa kufungua kesi ya mauaji dhidi ya watuhumiwa hao kutokana na kutopatikana kwa mwili wa Rufina Joseph, ambaye ni mama wa mtoto huyo.
Miili ya wanawake hao watatu, imefukuliwa ikiwa ni baada ya miaka mitatu kupita kutokana na ndugu na polisi kuamini kuwa, mojawapo ya miili hiyo unaweza kuwa wa mama huyo.
Mtoto wa mama huyo, aitwaye Caren kwa sasa analelewa Kituo cha Kulelea Watoto cha Upendo mjini Moshi, baada ya kuchukuliwa kutoka mikononi mwa Beatrice Massawe.
Habari zilizopatikana jana zilisema maiti za wanawake hao zilifukuliwa chini ya usimamizi wa madaktari na sampuli zake kutumwa Dar es Salaam kwa ajili ya kupimwa DNA.
Maiti hizo zilizikwa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga, baada ya kuhifadhiwa kwa siku zaidi ya saba na kukosa ndugu.
Mama mzazi wa Rufina, Magdalena Mwacha alilieleza gazeti hili jana kuwa maiti hizo tatu zilifukuliwa kwa ajili ya kupimwa DNA kuthibitisha kama moja ni ya mwanaye huyo.
“Tulienda Arusha na ile mifupa ilipimwa na mimi nikapimwa wakaniambia nisubiri watanieleza ni lini nichukue ile mifupa kwa ajili ya kuizika, maana ni ya mwanangu,” alisema Magdalena.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz jana alithibitisha kufukuliwa kwa maiti hizo na sampuli kutumwa Dar es Salaam.
“Ni kweli hizo maiti zilifukuliwa na wataalamu na sampuli zake zimetumwa Dar es Salaam kwa ajili ya kupimwa DNA, bado tunasubiri majibu hayo ya kitaalamu,” alisema Boaz.
Katika kesi ya wizi wa mtoto, inadaiwa kati ya Februari 10 na 16, 2010 Hospitali ya Kibosho, Moshi Vijijini watuhumiwa walimghilibu Rufina na kumwibia mtoto wake huyo.
Washtakiwa hao walikanusha, lakini upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Veritas Mlay uliwasilisha hati ya kiapo kupinga dhamana kwa washtakiwa.
“Uchunguzi kuhusu mahali alipo Rufina Joseph Mwacha bado unaendelea na upo katika hatua za mwisho na washtakiwa ndiyo watu wa mwisho kuwa na Rufina,” alidai Wakili Mlay.
Hata hivyo, baadaye mahakama ilitoa dhamana kwa washtakiwa hao na kesi hiyo sasa inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Gabriel Shayo na kuendeshwa na Wakili Tamari Mndeme.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment