Home » » Rehema Matowo, Mwika

Rehema Matowo, Mwika


KUFUATIA kero ya ubovu wa barabara waliyokuwa wakipata wananchi wa Kijiji cha Mrimbo Uuwo, Kata ya Mwika Kaskazini, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, hatimaye wameamua kuitengeneza kwa nguvu zao.

Wananchi hao waliamua kuchukua uamuzi huo baada ya barabara za kijiji hicho zenye urefu wa kilomita 12.3 kupitika kwa shida, huku nyingine kutopitika kutokana na mashimo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rumishaeli Mariki, alisema matengenezo hayo yako chini ya mradi wa barabara wa kijiji unaotegemea fedha kutoka kwa wananchi.

 “Tulikaa kwenye mkutano mkuu wa kijiji na tukapitisha maazimio kila kaya ichangie Sh5,000 kwa ajili ya kutengeneza barabara zetu, ambazo zimeharibika na zinapitika kwa shida, wananchi walipokea jambo hilo na tayari wamechanga Sh1.3 milioni,” alisema Mariki.

Mariki alisema kijiji hicho kina kaya 1,150 na kwamba, wanaanza kukarabati kilomita tano kwa kuchimba na kushindilia kwa kutumia katapila, kadri fedha zitakapopatikana ndivyo barabara nyingine zitafanyiwa matengenezo.

Alisema barabara hizo ni muhimu kwa shughuli za biashara, lakini zaidi zimekuwa zikitumika kwa wananchi kwenda Zahanati ya Uuwo kupata huduma ya afya na kusafirisha mazao yao kutoka mashambani.

Alisema kila mwaka wamekuwa wakiziombea ruzuku barabara hizo, kutoka halmashauri lakini hakuna mafanikio ndiyo maana wameamua kutumia nguvu zao ili Serikali iwaunge mkono.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa