Home » » ASKARI APOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA GARI

ASKARI APOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA GARI


Na Upendo Mosha, Moshi
ASKARI mwenye namba D.8384 CPL Julias Kimathi, amefariki dunia mkoani Kilimanjaro, baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana uso kwa uso na fuso lenye namba za usajili T.553 AJN .

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Robert Boaz, alisema tukio hilo lilitokea Agosti 26 mwaka huu, saa saba usiku katika eneo la Chekereni Wilaya ya Moshi Vijijini.

Alisema Mitsubishi Fuso yenye namba T.553 AJN lililo kuwa likitokea Arusha kwenda Tanga, liligongana uso kwa uso na Toyota Pickup yenye namba 781 AHZ iliyokuwa ikiendeshwa na askari huyo.

Kamanda Boaz alisema, inadaiwa magari hayo yaligongana baada ya dereva wa FUSO aliyekuwa akijaribu kulipita Trekta aina ya Messey Ferguson, kushindwa kulimudu gari lake ndipo alipokwenda kugongana na gari la askari huyo.

Alisema kuwa, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa fuso kutaka kulipita trekta hilo bila kuchukua tahadhari ya kutosha.

Wakati huo huo Kamanda Boaz aliwataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kazi ya Sensa, inayoendelea nchi nzima na kuwataka wananchi ambao bado hawaja hesabiwa kutimiza wajibu huo muhimu.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa