Home » » DAWA ZA KULEVYA ZENYE THAMANI YA SH MILIONI 447 ZAKAMATWA

DAWA ZA KULEVYA ZENYE THAMANI YA SH MILIONI 447 ZAKAMATWA

Na Upendo Mosha, Moshi
DAWA za kulevya zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 447 zimekamatwa katika kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka huu, mkoani Kilimanjaro, zikiwa na uzito wa zaidi ya kilo 1,102.

Akizungumzia kukamatwa kwa dawa hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema aina ya dawa hizo zilizokamatwa ni bangi, cocaine, heroine na mirungi.

Alisema kutokana na dawa hizo kukamatwa, zaidi ya kesi 383 zimefikishwa mahakamani na zaidi ya watu 323 wameshikiliwa ambapo kati yao wanaume ni 280 na wanawake wakiwa 43.

Alisema bangi zilizokamatwa ni kilo 421,238 zenye thamani ya Sh 42,100,000, kilo 7.787 za cocaine zenye thamani ya Sh 371,346,000, kilo 0.9 za heroine zenye thamani ya Sh 24,800 na kilo 673.41 za mirungi zenye thamani ya Sh 33,650,000.

Alisema kati ya kesi 383, watuhumiwa wa jumla ya kesi 80 walipatikana na hatia na vifungo na wengine kulipa faini ya jumla ya Sh 2,360,000 na watuhumiwa watatu waliachiwa huru.

“Katika kipindi cha Januari hadi Julai, mwaka huu, tumeweza kupeleka kesi 383 mahakamani na kuwakamatwa wanawake 43 pamoja na wanaume 280, idadi hii inatisha katika hali ya kawaida, ila Jeshi la Polisi tumejipanga vyema kukabiliana na biashara hii ya uingizwaji wa dawa nchini,” alisema Boaz.

Alisema uingizwaji wa dawa hizo ni janga kubwa kwa vijana na aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa ajili ya kutokomeza biashara hiyo na iwapo watamtilia shaka mtu yeyote watoe taarifa haraka.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa