Home » » ASKARI WADAIWA KUACHIA WAHAMIAJI HARAMU 14

ASKARI WADAIWA KUACHIA WAHAMIAJI HARAMU 14


na Charles Ndagulla, Moshi
ASKARI wa Kituo cha Polisi Himo na maofisa Uhamiaji katika kituo cha Holili, mkoani Kilimanjaro wanatuhumiwa kuliachia gari lililokamatwa likiwa limepakia wahamiaji haramu 14 kutoka nchini Eithiopia.
Uchunguzi uliofanywa na TanzaniaDaima umebaini gari hilo T 324BRG Noah lilikamatwa na maofisa hao wa serikali Julai 27 mwaka huu, majira ya saa sita usiku katika eneo la Njiapanda katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo.
Maofisa hao wa polisi wakishirikiana na maofisa wa Uhamiaji kutoka Holili, walilizingira gari hilo na kulifanyia upekuzi na baada ya kuwakuta wahamiaji hao haramu waliwachukua na kuwaingiza kwenye gari la Mkuu wa Kituo cha Polisi Himo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wahamiaji haramu hao wakisafrishwa kutoka Njiapanda kwenda Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi bila kuwapo kwa gari lililokuwa limewabeba.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, ameonekana kujikanganya katika utoaji wa taarifa ya kukamatwa kwa Waethiopia hao baada ya kushindwa kutoa ufafanuzi juu ya mazingira ya kukamatwa kwao.
Katika taarifa yake isiyokuwa na nembo ya Jeshi la Polisi wala saini yake, Kamanda Boaz alidai wahamiaji hao walikamatwa eneo la Njiapanda Chekereni bila kufafanua walikuwa wakifanya nini ama walikuwa katika mazingira gani.
Uchungunzi zaidi umebaini eneo lililotajwa na Kamanda Boaz ni maeneo mawili tofauti, kwani kuna umbali wa kilometa mbili kutoka Njiapanda hadi Chekereni, hivyo huwezi kuunganisha jina moja la Njiapanda Chekereni.
Kumekuwapo na tuhuma kuwa magari aina ya Noah ambayo kwa sasa ndiyo hasa yamekuwa yakisafirisha wahamiaji haramu kutoka Taveta nchini Kenya, mengi kati ya hayo yanamilikiwa na askari wa Jeshi la Polisi katika miji ya Tarakea, Holili, Himo na Moshi mjini.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa