Home » » KKKT KUKUTANA NA WATUMISHI WALIOGOMA KCMC

KKKT KUKUTANA NA WATUMISHI WALIOGOMA KCMC

Na Arodia Peter
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) nchini, limeanza kazi ya kutoa ushauri kwa watumishi wake waliopo katika hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro.

Hayo yalielezwa jana na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk. Alex Malasusa, katika Ibada maalum ya ufunguzi wa jengo la Kanisa lililoko Mabibo Farasi mjini Dar es Salaam.

Dk. Malasusa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alisema, wakati huu ambao nchi inapita katika kipindi cha mpito na kushuhudia migomo mbalimbali ikiwemo ya madaktari, Kanisa limeona kuna haja ya kukaa na watumishi ambao pia ni waumini wa KKKT waliopo KCMC, ili waweze kufanya kazi kwa moyo na kusaidia Watanzania.

Alisema mikutano mbalimbali kwa watumishi hao, imeanza wiki iliyopita ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Jubilei ya miaka 120, toka kuanzishwa kwa kazi ya Injili hapa Tanzania.

“Hiki ni kipindi cha mpito kwa nchi yetu kushuhudia migomo ya kila aina, ikiwemo ya madaktari, KKKT kama wadau wakuu katika hospitali ya KCMC, tumeona ni vema tufanye mikutano na watumishi waliobaki, ili waendelee kuwahudumia Watanzania,” alisema Askofu Malasusa.

Ujenzi wa Kanisa hilo jipya lilianza Novemba 15, 2006 kwa michango mbalimbali ya waumini na limegharimu kiasi cha Sh millioni 627.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa