Home » » MAKARANI WA SENSA KUFANYISHWA MTIHANI

MAKARANI WA SENSA KUFANYISHWA MTIHANI


Na Eliya Mbonea, Hai
MAKARANI wa Sensa katika Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, wanatarajiwa kufanyishwa mtihani wa kuwapima ili kuona kama wameelewa kile walichofundishwa kwa nadharia na vitendo katika mafunzo yao.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga juzi, alipofungua mafunzo ya wasimamizi na makarani wa Sensa ya watu na makazi kwa Wilaya ya Hai ambapo makarani 644 walishiriki.

Makunga alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa vyama vya siasa na Serikali wilayani humo kutoa ushirikiano katika kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa wananchi kushirikiana na makarani hao.

"Wananchi wanapaswa kuendeleza ushirikiano na mshikamano kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika masuala mengine ya kitaifa kwa kuhakikisha sensa inafanyika kwa ufanisi," alisema Makunga.

Makunga alibainisha kwamba tayari utaratibu ulishaandaliwa wa kufanyika zoezi la uhamasishaji katika maeneo yote litakalofanywa na madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na kamati ya sensa ya wilaya.

Alisema ni muhimu kwa makarani wote kuheshimu dhamana kubwa waliyopewa na Serikali, kwa kuwa miongoni mwa wananchi 2,700 walioomba kufanya kazi ya sensa kwa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

"Ni muhimu mtumie elimu mtakayoipata katika mafunzo haya, busara na uwezo wenu wote kutambua maeneo ya kuhesabia watu, mbinu za kuuliza maswali na kujaza madodoso katika ngazi ya kaya, kuhakiki na kutunza madodoso,” alisema.

Aidha Makunga alitumia nafasi hiyo kufafanua madai yaliyoenezwa na baadhi ya watu wilayani humo kuwa serikali inawachukia walimu na ndiyo maana haikuwapa nafasi katika zoezi la sensa

Akielezea zaidi katika kundi hilo la makarani, Makunga alisema sehemu kubwa ni walimu ambao ni 340, huku wengine wakiwa wahitimu wa kidato cha nne, sita na vyuo vikuu na wachache ni watumishi wa umma.

“Tungependa kuchukua watu wote 2,700 walioomba, lakini kwa bahati mbaya nafasi ni 644, hivyo katika hizo chache tumehakikisha tunachanganya makundi yote, yakiwamo ya wazoefu na wasiokuwa na uzoefu,” alifafanua Makunga.

Naye Mwenyekiti wa makarani hao, Fadhili Simbano, alimhakikishia mkuu huyo wa wilaya kwamba kutokana na umakini mkubwa wa kuteua makarani, wilaya hiyo itakuwa miongoni mwa wilaya ambazo zitafanya zoezi hilo kwa ufanisi mkubwa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa