Home » » MTENDAJI AKWAMISHA MAENDELEO

MTENDAJI AKWAMISHA MAENDELEO

na Rodrick Mushi, Moshi
WANANCHI wa Kijiji cha Mdawi, Kata ya Kimochi, Wilaya ya Moshi Vijijini, wamemlalamikia Mtendaji wa kijiji hicho, Lenard Mende kwa kushindwa kuwepo ofisini siku za kazi, pamoja na kuwa mtoro kwenye mikutano ya serikali, ambayo inakuwa na lengo la kujadili shughuli za maendeleo.
Wakizungumza baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa kijiji na kuahirishwa bila kujadili agenda yoyote, wananchi waliokuwa wamehudhuria walisema kuwa hiyo ni mara ya pili kushindwa kufanyika.
Walisema Julai 8 mwaka huu, mtendaji huyo aliondoka kwenye mkutano baada ya kuulizwa swali na mmoja wa wananchi.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mdawi, Rumisha Kinyaa aliwaeleza wananchi waliokuwa wamefika kwenye mkutano huo ulioahirishwa Agosti 4, mwaka huu kuwa, walikuwa wamempa taarifa ya uwepo wa mkutano huo Mtendaji wa Kijiji, lakini hadi kufika muda wa mkutano, hakuwa ametokea.
Alisema kuwa hawataweza kuendelea na mkutano huo, kwa kuwa agenda mbalimbali ambazo zingejadiliwa kwa siku hiyo, ingekuwa ni kazi bure bila kuwepo kwa mtendaji.
“Miongoni mwa mambo ambayo wananchi walikuwa wahoji kwenye mkutano huo, ni pamoja na kutokufika kwa mtendaji huyo ofisini siku za kazi, jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwa wanakijiji, wakati yeye ameletwa kwa ajili ya kushirikiana nao kuleta maendeleo,” alisema Kinyaa.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kimochi, Anamenyisa Macha alisema kuwa changamoto nyingi zinazotokea kwenye kijiji hicho zinatokana na itikadi za kisiasa ambazo zinasababishwa na mvutano wa vyama vya siasa, pamoja na wananchi kupingana na kugawa kijiji cha Mdawi.
Alisema, kinachotakiwa ni wananchi na viongozi kuondoa itikadi zao na kuwatumikia wananchi, ili kuweza kuleta maendeleo, pamoja na kuchunguza malalamiko yalipo kwa wananchi kuwa hawakuhusishwa katika ugawaji wa kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ibrahim Msengi alipoulizwa kuhusiana na tatizo lililopo kwenye kijiji hicho, alisema kuwa amebanwa na shughuli za mbio za mwenge ambao ulikuwa mkoani Kilimanjaro, huku akiahidi kulifuatilia suala hilo baada ya kumalizika kwa mbio hizo.
Naye Mtendaji wa kijiji anayelalamikiwa, Mende, alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia madai hayo dhidi yake, alisema yupo kwenye eneo lenye kelele, hivyo asingeweza kuwasiliana vizuri na mwandishi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa